Mbunge wa Mbulu Vijijini (CCM), Flatei Massay amehoji ni lini Serikali itasaini mkataba wa ujenzi wa barabara ya kutoka Haydom au hadi aruke sarakasi kwa namna nyingine bungeni.
Endapo ataruka sarakasi wakati wa uwasilishaji wa bajeti ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi Jumatatu ijayo, itakuwa ni mara ya pili baada ya kufanya hivyo kwenye bajeti ya wizara hiyo ya mwaka 2022/23, Mei 23, 2022.
Amesema mwaka jana walipitisha bajeti ya kujenga kipande cha Haydom kwa kiwango cha lami.
“Na bajeti yako bado hatujapitisha lini utasaini mkataba ili kipande kile kijengwe kwa kiwango cha lami ama tuje kwa sarakasi kwa namna nyingine tena kwenye bajeti hii ya Jumatatu,”amesema.
Akijibu swali hilo Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Atupele Mwakibete amesema kabla ya mwaka 2022/23 kuisha ana uhakika watakuwa wamesaini mkataba ili mkandarasi aweze kuanza kazi ujenzi wa barabara hiyo.