Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima amewashauri wanawake na wanaume wasioe au kuolewa kwa kufuata mkumbo.
Dk Gwajima alisema hayo wakati wa kuadhimisha Siku ya Familia Duniani na akihimiza wanaume watimize majukumu yao kama baba kwa vile wao ni kichwa cha familia.
Dk Gwajima amesema watu wasiingie kwenye ndoa kwa sababu ya fulani kaolewa/ kaoa na kwamba kufanya hivyo ni kutengeneza machozi yao wenyewe.
“Niwatie moyo, kwanza tukumbuke tuingie kwenye ndoa kwa mpango, si mtu akitoka yuko na mkewe au mumewe na wewe unaona uingie unasema mimi nitaonekanaje huko ni kujitengenezea machozi mwenyewe,” amesema.
Dk Gwajima amesema mwanaume ama mwanamke anapoingia kwenye ndoa lazima achague rafiki ambao lengo lao ni moja na hapo atakuwa amejipunguzia athari za kuingia kwenye machozi.