
Wakati Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha), wakiandamana kina Halima Mdee waondolewe bungeni, mbunge huyo amesema hao ni ‘watoto wa juzi na hawajui alikotoka’.
“Unajua watoto hawatakiwi kunyimwa usingizi, ndio maana siwajibu wengi wanaopiga talalila ‘kelele’ wamenikuta mjomba napiga mzigo pale (Chadema). Wametamani baada ya mzigo kutema, ukishakuwa mkubwa huwezi kuangaika na watoto, wanasema unawaacha,”amesema Mdee.
Mdee aliyewahi kuwa mwenyekiti wa Bawacha kwa nyakati tofauti ameeleza hayo leo Jumanne Mei 16, 2023 wakati akihojiwa na Wasafi TV jijini Dodoma. Katika maelezo yake, Mdee amesisitiza kuwa yeye bado ni Chadema ‘for life’.
Katibu Mkuu wa Bawacha, Catherine Ruge amemjibu kwa kusema sio sahihi kuzungumza kauli kama hizo, hata hivyo, akasema waswahili wana msemo unaosema ‘mfamaji haishi kutapa tapa.’ Ruge amedai Mdee ameonesha dharau kwa Bawacha kusema waliondamana ni watoto.