Mtu aliyefahamika kwa jina la Benedicto Modest Mangi aliyekuwa dereva bajaji ya mizigo, Mkazi wa Mtaa wa Usule, Kata ya Mbugani Manispaa ya Tabora ameuawa kwa kupigwa na kitu kizito kichwani kisha mwili wake kufukiwa kwenye shimo tukio linalohusishwa na wivu wa mapenzi linalodaiwa kufanywa na mtu mmoja ambaye ni utingo wake waliyekuwa wakifanyakazi pamoja.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, ACP Richard Abwao amethibitisha tukio hilo na kuwaeleza waandishi wa habari kwamba mtuhumiwa ambaye jina lake linahifadhiwa anadaiwa kufanya mauaji hayo kufuatia kumtuhumu dereva wake wa bajaji kwamba amekuwa na uhusiano wa kimapenzi na mkewe.
Kamanda Abwao amesema Utingo huyo ambaye yupo mikononi mwa Jeshi la Polisi akihusishwa na mauaji hayo inadaiwa aliwahi kumuonya dereva wake kwa kumtaka aachane na tabia hiyo kabla ya kujichukulia sheria mkononi kwa kufanya mauaji hayo walipokuwa wanakwenda kijijini kubeba mzigo.
Inadaiwa baada ya kutekeleza mauaji hayo utingo huyo alichimba shimo kisha kuufukia mwili wa dereva wake na kutokomea siku moja kabla ya Polisi kufanikiwa kubaini tukio hilo na kumkamata mtuhumiwa.
