Jeshi la Polisi jijini Jinja, Uganda wamemkamata mwalimu wa kike wa Shule ya Wasichana ya PMM kwa madai ya kuendeleza ushoga shuleni. Msemaji wa polisi mkoani Kiira, James Mubi, alisema mwalimu huyo alikamatwa baada ya mwanamke anayedaiwa kuwa mpenzi wake kumshtaki kwa polisi.
Mpenzi wake alimtuhumu kwa kutomjali na kujihusisha na kuwasajili wasichana wadogo wa shule kujiunga na ushoga. “Mpenzi wake anayedaiwa kuwa Msagaji, mwenye umri wa miaka 30, alijisalimisha kwa polisi. Tuna wanandoa chini ya ulinzi wetu. Mwenzi huyo anadai mwalimu amekuwa akimlaghai na kutompatia mahitaji ya kimsingi.”
"Lakini mshukiwa alitoa ushahidi kwa polisi kwamba alimkodishia nyumba mpenzi wake na kumuanzishia biashara yake ya mbao na alipinga madai ya kutompa mahitaji ya kimsingi kwa mwenzake msagaji," Mubi alisema. Alisema kwa mujibu wa mpenzi wake, mwalimu huyo amekuwa na tabia za kiume na hata kuvalia kama wanaume.
Mubi alisema wawili hao watafikishwa mahakamani kwa mashtaka ya unyanyasaji wa kingono pindi uchunguzi wa kesi hiyo utakapokamilika.
Wazazi waandamana Hatua ya kukamatwa kwa mwalimu huyo inajiri baada ya mamia ya wazazi kufanya maandamano katika Shule ya Wasichana ya PMM jijini Jinja siku ya Ijumaa, Machi 3, kufuatia kuenea kwa madai kwamba mmoja wa mwalimu wa shule hiyo ni msagaji.
Wazazi hao waliokuwa na hasira za mkizi walimshutumu mwalimu huyo kwa kuwaharibu mabinti zao. Licha ya kuzuiliwa kuingia shuleni humo, wazazi hao waliamuru watoto wao waondolewe katika mabweni wakishikilia kuwa hawatakubali wanao kutumika kufanya ushoga. Walizua kwamba wanao walikuwa wakilipwa KSh3400 kujiunga na LGBTQ.