Mahakama Kuu ya Tanzania imeliamuru Gazeti la The Citizen kumlipa aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Nehemia Mchechu kiasi cha Tsh bilioni 2.5 kwa kuandika habari iliyomchafulia jina lake.
Katika adhabu hiyo, Tsh bilioni 2 ni kwa ajili ya kumlipa fidia kwa kuchafulia jina na kumshushia hadhi yake.
Hukumu hiyo imetolewa leo Mahakama Kuu, Masijala ya Dar es Salaam, ikielezwa kuwa gazeti hilo lilichapisha taarifa ambazo zilimtuhumu Mchechu juu ya matumizi mabaya ya fedha za umma na kutumia maneno yaliyoshusha hadhi yake, huku wakidai walinukuu maneno ya aliyekuwa Rais wa Tanzania, hayati Dkt. John Magufuli alipokuwa akizindua mradi wa nyumba za NHC zilizopo Dodoma mwaka 2017.
Mchechu ambaye wiki iliyopita aliteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa Msajili wa Hazina, alifungua kesi hiyo mwaka jana katika Mahakama Kuu ya Tanzania akilitaka gazeti la The Citizen kumlipa fidia ya Sh. bilioni 3 kwa madai ya kuandika habari zilizomchafua.
Katika kesi hiyo iliyoanza kusikilizwa Mei 13, 2022 mbele ya Jaji Leila Mgonya wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam Mchechu alidai toleo la Gazeti hilo la Machi 23, 2018, lilichapisha habari iliyosomeka ‘Why JPM dissolved NHC Board, sacked Mchechu’ ikiwa na tafsiri isiyo rasmi kuwa kwanini JPM alivunja Bodi ya NHC, kumfukuza Mchechu’.
“Habari hii ililenga kunichafua, kunishushia hadhi, kunikosanisha na jamii kubwa ya Watanzania na kuonekana kuwa ni mimi ni mtu nisiyefaa kabisa kuwa kiongozi au sehemu ya jamii njema ya Watanzania mtu nisiye na maadili, nisiyeaminika na kimsingi nisiyestahili hata kuongoza popote,” alisema Mchechu ambaye anawakilishwa na mawakili wa kujitegemea Aliko Mwamanenge na Vitalis Peter katika kesi hiyo.
Mchechu ambaye alirejeshwa katika nafasi yake na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan baada ya kuondoka mwaka 2018, alisema habari hiyo ina upotoshaji wa kimantiki na kimaudhui kwa kuwa hajawahi kufukuzwa kazi kama ilivyodaiwa.
“The Citizen liliandika habari ile likijua sijafukuzwa kazi na wala Mheshimiwa Rais (John Magufuli) hakuwahi kunifukuza kazi na hii ilikuwa ni habari ya uongo na yenye nia ovu ya kunichafua na kunishushia hadhi katika familia yangu, taifa na duniani kwa ujumla,” alisisitiza Mchechu.