Kiongozi wa Muungano wa Azimio la Umoja, Raila Odinga ametangaza kampeni ya kuanza kususia bidhaa kutoka baadhi ya kampuni za nchini humo zinazojihusisha na serikali inayoongozwa na Rais William Ruto.
Odinga amesema kampuni hizo zimekuwa zikishirikiana na utawala wa Kenya Kwanza kuwahujumu wafuasi wa Azimio na kuwataka wafuasi hao kususia ulaji wa mayai kama njia ya kuonyesha uasi wao dhidi ya utawala wa Rais Ruto.
Akiongea na wafuasi wake kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kaunti ya Migori Machi 10, Odinga aliweka wazi wanaanza kampeni za kukataa bidhaa moja baada ya nyingine na huduma za kampuni zinazohusishwa na serikali ya nchini humo.