Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Kanal Laban Thomas, ameagiza kung’olewa (kuondolewa) milango yote iliyofungwa katika Hospitali ya wilaya Nyasa na kituo cha Afya Kingerikiti wilayani humo, baada ya kubaini mbao zilizotumika kutengenezea hazina ubora unaotakiwa.
Kanal Laban ametoa agizo hilo kwa nyakati tofauti,baada ya kukagua ujenzi wa kituo cha Afya Kingerikiti ambapo ujenzi wake umefikia asilimia 95 na maendeleo ya ujenzi wa baadhi ya majengo katika Hospitali ya wilaya.
Laban,ametoa onyo kali kwa mafundi wanaojenga miradi mbalimbali ya maendeleo na kusisitiza kuwa,mkoa huo sio wa kujifunzia bali ni mkoa unaohitaji mafundi wenye uwezo na wanaofanya kazi kwa weledi ili miradi inayotekelezwa ilingane na thamani halisi ya fedha zinazotolewa.
“Haiwezekani hata kidogo fundi amekwenda kuokota mabanzi na kuja kutufungia kwenye jengo letu,jambo hili sikubaliani nalo hata kidogo,nakuagiza hakikisha unafanya marekebisho ya milango yote haraka tena kwa gharama zako”alisema.
Alisema,kamwe hawezi kukubaliana na mambo ya ovyo yanayofanywa na baadhi ya watendaji wa umma wanaoshindwa kutekeleza na kusimamia miradi ya maendeleo yenye lengo la kusukuma kasi ya kukua kwa uchumi wa mkoa huo na kuwataka watumishi wa Halmashauri ya Nya kuacha kufanya kazi kwa mazoea.
Alisema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan,imepeleka zaidi ya Sh.bilioni 1 katika wilaya hiyo kwa ajili ya kujenga vituo viwili vya afya vya Lipalamba na Kingerikiti ili kuimarisha huduma za afya kwa wananchi,hivyo hakuna sababu ya wananchi wa maeneo hayo kuendelea kukosa huduma.
Aidha Laban, ametoa wiki mbili kwa viongozi wa wilaya ya Nyasa, kuhakikisha wanamaliza ujenzi wa kituo cha Afya Kingerikiti ili wananchi waanze kupata huduma za matibabu.
“hiki kituo kilipaswa kukamilika tangu mwaka jana,lakini naona hadi leo hii ujenzi wake bado haujakamilika,sasa natoa wiki mbili mfanye marekebisho na kianze kutoa huduma”alisema Kanal Laban.
Akiwa katika Hospitali ya wilaya,Kanal Laban amesikitishwa kukuta milango yote inayoendelea kufungwa katika majengo ya kutolea huduma ikiwa imepishana na baadhi mbao zake zikiwa mbichi.
Mkuu wa mkoa wa Ruvuma,ameagiza fundi aliyetengeneza milango hiyo kutolipwa fedha hadi atakapofanya marekebisho kwa kuwa amekwenda kinyume na mkataba.
Majengo yanayojengwa ni mochwari,jengo la upasuaji kwa wanawake na wanaume na njia za watembea kwa miguu mradi unaotekelezwa kwa gharama ya Sh.milioni 800 ikiwa ni uendelezaji wa awamu ya tatu ya ujenzi wa Hospitali hiyo.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya hiyo Filbetho Sanga,amehaidi kufanyia kazi maagizo ya Mkuu wa mkoa na mapungufu yote yaliyobainika katika ujenzi wa miradi hiyo hasa milango.
Dc Sanga,amewataka wakandarasi wanaofanya kazi katika wilaya hiyo kuhakikisha kazi wanazofanya zinakuwa bora na hatopokea mradi wowote uliojengwa chini ya kiwango.
Mkazi wa kijiji cha Kingerikiti Zakari Mbele,ameiomba serikali kukamilisha haraka ujenzi wa kituo cha afya Kingerikiti ili waanze kupata huduma za matibabu karibu na makazi yao.