Mbunge wa Jimbo la Kongwa na Spika wa zamani wa Bunge, Job Ndugai amewataka wananchi kufanya kazi kwa bidii na kujiletea maendeleo badala ya kutumia muda mwingi kulalamika.
Akizungumza wakati wa mkutano wa baraza la madiwani kujadili bajeti ya Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA), Wilaya ya Kongwa, Ndugai amewaasa madiwani kuhamasisha wananchi kuitumia vema miundombinu iliyojengwa na serikali zikiwemo barabara kwa ajili ya kujiletea maendeleo.
Amesema kuwa jukumu la kwanza la serikali ni kulinda usalama wa wananchi hivyo ni wajibu wa wananchi kufanya kazi kwa bidii na kujiletea maendeleo badala ya kutumia muda mwingi kulalamika. Wakati huo huo, alitoa wito kwa wananchi kushiriki kikamilifu kwenye kampeni endelevu ya utunzaji wa mazingira kwa kuhifadhi ardhi, kupanda miti na kutunza miundombinu.