Kijana Laurence Nicholaus Mwangake mwanafunzi wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Rohila iliyopo Mbalizi Mkoani Mbeya amelazwa Hospitali ya Ifisi ikidaiwa amejeruhiwa vibaya na Walimu wanne pamoja na Walinzi wawili wa shuleni hapo.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Shule ya Rohila zinaelezwa kuwa chanzo ni baada ya Mwalimu kumtuhumu mwanafunzi huyo kudokoa maandazi manne, Jumapili ya Februari 12, 2023.
Baada ya mwalimu kumtuhumu akashirikiana na walinzi kuzuia mlango na dirishani ili mwanafunzi asiweze kutoroka, baada ya hapo wakaongezeka Walimu na kisha kuanza kumshambulia kwa kipigo.
Kipigo hicho kilisababisha majeraha makubwa kwenye mwili wa Mwanafunzi ndipo akapelekwa hospitali kwa ajii ya matibabu.
Baada ya kupata taarifa kuwa mwanafunzi huyo amelazwa inadaiwa Walimu wakageuza kibao na kudai mwanafunzi ameumia wakati akiruka dirishani baada ya tukio la wizi wa maandazi.
Taarifa ya kutoka Hospitali
Vyanzo kutoka Hospitali zinaeleza kuwa hali ya Mwanafunzi siyo nzuri na amelazwa tangu Jumapili, anasaidiwa na baba yake mzazi ambaye ndiye anayemuuguza hospitalini hapo.
Shule yamtaka mzazi alipe hasara
Chanzo kutoka shuleni kinaeleza kuwa licha ya kinachoendelea, shule imegeuza kibao na kumtaka baba wa mwanafunzi huyo alipe gharama za kioo cha dirisha ambacho wanadai mwanafunzi alikivunja wakati akitoroka baada ya kuiba maandazi.
Tamko la Polisi
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Benjamin Kuzaga, amesema: “Nimebanwa na shughuli nyingine za kiofisi, nina wageni, lakini ninawaagiza Wasaidizi wangu wafuatilie kisha kama kuna tukio la aina hiyo tutatoa taarifa rasmi.
Ofisi ya Afisa Elimu
Afisa Elimu Mkoa wa Mbeya, Ernest Hinju alipoulizwa kuhusu tukio hilo, amesema anaombwa atafutwe baadaye kwa kuwa ametuma wasaidizi wake kwenda kufuatilia.
Muuguzi wa Hospitali aeleza
Mmoja wa wauguzi wa kike ambaye amempokea mgonjwa huyo amesema “Aliletwa hapa akiwa hayupo vizuri kiafya, ana majeraha yanayoonekaa ni ya kupigwa eneo la uso, mguuni na mikononi.
“Anahudumiwa na baba yake ambaye ndiye anayemsaidia kumuogesha na kumpa huduma nyingine ambazo ni za binafsi sana.”
Aidha ameongeza "Kuna maofisa kadhaa nadhani ni kutoka ofisi ya Afisa Elimu, naona wamefika hapa na kumtafuta huyo kijana."
Tamko la mganga mkuu
Akizelezea hali ya mgonjwa, Mganga Mkuu wa Hospitali ya Ifisi, Dkt. Hamis Bakari Ally anasema: “Mgonjwa anaendelea vizuri, hali yake ni vizuri kiasi, ana maumivu ya mguu kwenye goti, ameeleza aliumia wakati anaruka kutoka kwenye chumba alichofungiwa, hali ya kichwa ipo sawa, hakuna mvunjiko wowote.
“Hivyo majeraha mengine aliyonayo yalitokea wakati aliporuka kutoka kupitia dirishani wakati akijaribu kutoka kwenye chumba alichofungiwa.
“Watu wa shuleni kwake ndio waliomleta, kuhusu gharama za matibabu ana bima ya NHIF ndiyo anaitumia.”
Alipoulizwa kuwa kama chanzo ni kushambuliwa kwa vipigo kutoka kwa Walimu na Walinzi kama inavyodaiwa, Dkt. Hamis amesema: “PF3 ipo, tunayo kwenye faili letu la hospitali."
Kuna tamko lolote kutoka shuleni au kwenye mamlaka?
Dkt. Hamis: “Hapana hakuna tamko lolote kutoka shuleni, zaidi maafisa wa ofisi ya Afisa Elimu wamefika hapa na kumuona mgonjwa kisha wakasema wanaendelea na uchunguzi wao wa ndani kwa ndani."
Je, ni kweli mwanafunzi alidokoa maandazi?
Dkt. Hamis: "Tumezungumza naye mwanafunzi kwa kuwa sisi madaktari huwa tunauliza chanzo cha majeraha, amesema ni kweli aliiba maandazi kwenye kiduka cha shule, kwa kuwa alikuwa na njaa, ndipo akakamatwa. Mwanafunzi mwenyewe anasema alipoona adhabu imezidi ndipo akaruka dirishani ili kukimbia na ndipo majeraha yakaongezeka."
Chanzo:Jamii Forums