Mfugaji aliyetambulika kwa jina la Samweli Bulunde, anadaiwa kufariki dunia baada ya kujinyonga kwa kutumia nguo yake ya ndani (kaptula) akiwa kwenye Kituo cha Polisi Kanoge, Halmashauri ya Nsimbo mkoani Katavi.
Ni tukio linaoendana na upinzani wa hoja kutoka kwa familia ya marehemu, inayodai kuwapo maswali mengi yasiyo na majibu kuhusu alivyokamatwa, kifo chake kilivyotokea, kutokuwapo uthibitisho unaotolewa na mamlaka husika na kuhifadhiwa kituo cha polisi cha mbali na hapakuwapo taarifa zozote kwao.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Ali Makame, akitoa ufafanuzi kuhusu kifo hicho jana, alidai kuwa mtuhumiwa alichukua uamuzi huo akiwa mikononi mwa polisi, akituhumiwa kuhusika na mauaji na kukodi watu kwa ajili ya kutekeleza mauaji.
Alidai kuwa baada ya mtuhumiwa kuhojiwa kuhusu tuhuma hizo, alikiri kutekeleza matukio matatu ya mauaji mwaka 2020 na 2022, pia kutoa Sh. 500,000 kwa ajili ya kukodi watu wa kutekeleza mauaji.
"Ni kweli tukio hilo lipo na limetokea ila tu inatakiwa mjue Jeshi la Polisi lina mbinu nyingi za kumkamata mtuhumiwa.
"Alikamatwa Febuari 5 na Febuari 6 alichukua uamuzi wa kujinyonga kwa kutumia mshipi wa kaptula yake ya ndani na alisema ndugu zake wasijue kama alikuwa ni mtu wa namna hiyo.
"Lakini kwa kuwa ndugu zake walikuja hapa na wakataka kujua, tuliwaambia na wao wakabaki wanashangaa, hawakuamini kama ndugu yao alikuwa na mambo hayo, tuliwaambia kama hawaamini amejinyonga, basi walete daktari wao aje apime mwili.
"Lakini mpaka sasa wameelewa na wamekubali kuchukua mwili kwenda kumzika ndugu yao mkoani Mwanza," alisema Kamanda Makame.
Kabla ya kuchukua mwili huo, ndugu wa marehemu walionyesha kutoridhishwa na chanzo cha kifo cha ndugu yao, hivyo walifunga safari mpaka kwenye Ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi kujua kwa undani kilichomsibu ndugu yao.
Sama Kafalasa, msemaji wa familia hiyo, alidai: "Samweli Bulunde alikamatwa Febuari 5 mwaka huu eneo la Luhafye Tanganyika baada ya kupigiwa simu na Mwenyekiti wa Mtaa kuwa analalamikiwa na OCS (Mkuu wa Kituo cha Polisi) aliyefika pale.
"Yule mzee walishindwana na baadaye Mwenyekiti akataka apate taarifa ya kina kuhusu kukamatwa kwake.
"Basi OCS baada ya kutumia nguvu kumkamata, Mwenyekiti ilibidi awaachie ofisi lakini kweli mzee walimchukua na kumpeleka, siku iliyofuata tulijitahidi kufika kila kituo cha mkoa huu, hatukumpata hata kwenye rejista ya kipolisi.
"Baada ya siku kadhaa kupita huku tukiendelea kufuatilia, tuliambiwa mzee alijinyonga ndani ya kituo cha polisi.
"Sisi mnavyotuona hapa, wote ni familia moja, tumeona sasa tujiridhishe kwa Mkuu wa Mkoa, inawezekana alilifanya hilo maana na yeye ni mtu, na sisi tujiridhishe kwa madaktari wetu, hata kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa apimwe tuone kama hajaathiriwa na yule bwana ili nasi kama familia tukachukue mwili wa marehemu."
Mwenyekiti wa Mtaa wa Luhafwe, Rafael Nkuba alisimulia kuwa Febuari 5 mwaka huu, majira ya saa 11 jioni, alipigiwa simu na familia ya marehemu akiwa pamoja na aliyefikwa na umauti, wakimjuza kuwa walikuwa ofisini kwake na alipofika aliwakuta watu watatu ambao ni mtoto wa marehemu, mjukuu wa marehemu na mzee wao ambaye baadaye alidaiwa kujinyonga kwenye mahabusu ya polisi.
Baada ya kufika walimweleza kuwa asubuhi wamepigiwa simu na askari polisi lakini kabla ya hapo askari huyo aliwahi kufika ofisini kwa mwenyekiti huyo akimlalamikia mzee huyo kuwa amemjibu maneno mabaya, hivyo amwite ofisini kwake waje wazungumze.
Hivyo, alimpigia simu akamwambia mzee huyo alikuwa amesafiri na akamjulisha askari huyo na baada ya mwezi mmoja kupita, ndipo walimpigia simu hiyo ya kuwa walikuwa ofisini kwake.
"Basi nilimpigia afande akaja, alikuja na askari mgambo wawili, mmoja ninamtambua, mmoja simtambui kwenye kijiji changu kama mgambo. Basi, baada ya kufika pale, akatumia mamlaka, akasema 'mwenyekiti huyu ni mtuhumiwa wangu', nikashangaa 'amekuwa mtuhumiwa wako tena? Kivipi we si mlalamikaji? Lile tatizo ambalo ulikuja kumlalamikia yule mzee ueleze, wajumbe wapo tutawashauri yaishe'.
"Akasema 'mimi tayari nimeshapiga simu mkoani wanakuja kumchukua, basi nikaona mimi sina haja sasa ya kuwasikiliza maana hii ni ofisi yangu, huwezi kumfunga pingu huyu mtuhumiwa bila mimi kujua kosa.
"Ninafikiri alimfunga kwa nguvu, mimi ikabidi niondoke, niache ofisi wazi. Baada ya hapo, askari wa mkoani (Mpanda) kweli walifika wakamchukua.
"Sasa mimi kama mwenyekiti sikujisikia, tunaonekana sisi wa mamlaka ya chini hatuna nguvu ya kuongoza na hatuna nguvu ya kumzuia askari kwamba hili usilifanye akakuelewa.
"Mimi siku ya tukio nilitoa taarifa kwa (Ofisa) Mtendaji Kata na kwa diwani kabla hawajaja kumchukua, nao walikuwa na taarifa," alisimulia mwenyekiti huyo.
Kwa mujibu wa kiongozi huyo wa mtaa, Bulunde alikamatwa Febuari 5 mwaka huu na kudaiwa alijinyonga siku iliyofuata.
Alidai kuwa Febuari 13 mwaka huu, ndugu walifika kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ambako hawakuonana naye, lakini wakapatiwa maelekezo ya kwenda kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa kupatiwa ufumbuzi.
Muda mfupi baadaye, Nipashe iliyokuwa na wanafamilia hao ilishuhudia wakikubaliana kutafuta daktari wao atakayetoa majibu ya chanzo cha kifo cha ndugu yao.
Hata hivyo, jioni ya siku hiyo mwandishi wetu alipowasiliana na wanafamilia hao, kabla ya kutekeleza walichokubaliana, wakawa na uamuzi mpya wa kuufuata mwili wa marehemu kwa ajili ya maandalizi ya mazishi.
Wanafamilia hao waliuchukua mwili wa marehemu hospitalini mjini Mpanda ulikokuwa umehifadhiwa Jumatatu iliyopita, na kuanza kuusafirisha kwenda mkoani Mwanza kwa ajili ya maziko baada ya kukamilisha shughuli za kuuaga.
Chanzo: Nipashe