Wajifungua kwa kutumia mwanga wa tochi ya simu


Wananchi wa Kijiji cha Ndapata Kata ya Mlembwe wilayani Liwale, wameomba serikali iwasaidie kuwaletea umeme katika zahanati ya kijiji hicho, kwani wajawazito wamekuwa wakizalishwa na wakunga kwa kutumia mwanga wa simu.


Hayo yamesemwa jana na wananchi na viongozi wa kijiji hicho katika mkutano wa hadhara kijijini Ndapata kwa Mbunge wa Jimbo la Liwale, Zuberi Kuchauka ambaye alifanya mkutano huo kwa ajili ya kusikiliza kero za wananchi.

“Chumba cha wajawazito kujifungulia watoto hakina mwanga kwa sababu sola imepoteza uwezo wake wa kutoa mwanga katika ofisi ya zahanati hiyo, hali inayosababisha wakunga kutumia tochi au mwanga wa simu kuwapa huduma ya kujifungua wajawazito …” alisema Diwani wa Kata ya Mlembwe, Mohamed Mahangabane.

Kwa upande wake Mbunge Kuchauka alisema amesikia kilio chao na akamuagiza ofisa Mtendaji wa Kijiji amtafute mtaalamu akafanye tathimini ya bei ya sola na gharama za ukarabati wa miundombinu ya mfumo wa umeme katika zahanati hiyo, kisha wampelekee atalitatua tatizo hilo.

” Nimeguswa na hii changamoto inayoikabili zahanati yenu kwani ni wazi wanaoteseka ni wajawazito na wahudumu wa afya, kwani wajawazito wanazalishwa kwa kutumia mwanga simu …

“Hali hiyo inawasababisha wahudumu wa afya kufanya kazi katika mazingira magumu, hivyo naagiza tathmini ya bei ya sola ifanywe niletewe nitagharamia kiasi hicho cha fedha, ili umeme urejee katika zahanati ya Ndapata.

Wakati huohuo Kuchauka ameichangia serikali ya Kijiji sh 500,000 kulipia deni la jenereta kwa ajili ya kusaidia kupampu maji kutoka kisimani, ili wananchi waweze kupata maji kwani wanakabiliwa na tatizo la maji.

Chanzo: Habarileo


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo