RAIS
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan ametoa zaidi ya shilingi bilioni 60 kujenga
kilometa 35 za lami wilayani Mbinga mkoani Ruvuma.
Akitoa taarifa ya
ujenzi huo kwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma,Meneja wa TANROADS Mkoa wa
Ruvuma,Mhandisi Ephatar Mlavi amesema mradi huo
unahusisha ujenzi wa barabara ya lami ya Kitai hadi Lituhi yenye urefu wa kilometa 82.
Hata hivyo amesema kiasi cha fedha kilichotolewa na
serikali kinahusisha ujenzi wa barabara ya lami kwa kipande cha kutoka Kijiji cha Amanimakoro hadi Kijiji cha Ruanda,barabara yenye urefu wa kilometa 35.
Ameutaja mradi huo kuwa ulianza kutekelezwa Juni 15,2022 ambao unatarajiwa kutekelezwa kwa miezi 18, hivyo
kukamilika Desemba 2023 ambapo amemtaja Mkandarasi wa mradi huo kuwa ni kampuni
ya China Railway Seventh Group.
Amesema mradi huo unahusisha ujenzi wa kilometa 35 za
barabara kwa kiwango cha lami,ujenzi wa madaraja manne,ujenzi wa makalaveti
makubwa saba na ujenzi wa makalavati madogo 58 na kwamba hadi sasa ujenzi
umefikia asilimia 24 .Tayari serikali imetoa fedha za kujenga kilometa 40 kati
ya 82 .
“Barabara hii ina umuhimu mkubwa katika usafirishaji
wa makaa ya mawe kwa sababu eneo hili lina migodi mingi ya madini hayo hivyo
barabara hii itasaidia usafirishaji wa makaa ya mawe Kwenda sehemu mbalimbali
nchini ikiwemo bandari ya Mtwara’’,alisisitiza Mhandisi Mlavi.
Akizungumza mara baada ya kukagua mradi wa barabara
hiyo,Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma,Kanali Laban Thomas amempongeza Mkandarasi kwa
kufanya kazi ndani ya mkataba ambapo amesisitiza kazi hiyo ikamilike mapema ili
wananchi waanze kunufaika nayo.
Ameitaja barabara ya Kitai-Lituhi kuwa ni miongoni mwa
barabara kubwa mkoani Ruvuma yenye urefu wa kilometa 82 ambayo inategemewa na
Mkoa katika kukuza uchumi na kwamba inaunganisha wilaya za Mbinga na Nyasa ,pia
inaunganisha Mkoa wa Ruvuma na Njombe kupitia wilaya ya Ludewa.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma amemshukuru Rais Dkt Samia
Suluhu Hassan kwa kuchukua uamuzi wa kizalendo
wa kutekeleza mradi huo unaoufungua Mkoa wa Ruvuma kupitia barabara ya
Kitai-Lituhi.
Imeandikwa na Albano Midelo wa Kitengo cha
Mawasiliano Serikalini Mkoa wa Ruvuma
Januari 10,2023