Profesa wa Chuo Kikuu Sokoine cha Kilimo (SUA) kilichopo Mkoani Morogoro, Christopher Kasanga na mwenzake Linael Makundi mfanyakazi wa Benki ya CRDB Tawi la Mandela mkoani hapo wamefikishwa Mahakama ya Wilaya ya Morogoro kwa shtaka la madai ya Ugoni dhidi ya mlalamikaji Matrida Sigaret.
Akizungumza nje ya Mahakama hiyo jana, wakili wa mlalamikaji Emmanuel Chengulo alisema kesi hiyo ilifunguliwa Desemba 16, 2022 na ilitajwa kwa mara ya kwanza Januari 23, 2023 mbele ya Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Emmanuel Lukumai.
Aidha, wakili Chengulo amesema katika shtaka hilo Matrida Sigaleti anawashtaki Profesa Kasanga ambaye ni mume wake wa ndoa na Linael kwa kesi ya Ugoni dhidi yao.
"Kimsingi mteja wangu anadai kulipwa fidia ya shilingi milioni 100 kutokana na madhara ambayo ameyapata," alisema.
Wakili huyo alisema kuwa Oktoba 29, 2022 inadaiwa washtakiwa hao walifunga ndoa huku kukiwa bado kuna ndoa nyingine ya mlalamikaji ambaye ni Matrida na Profesa Kasanga.
Kwa upande wa washtakiwa ambaye ni Profesa Kasanga na Linael Makundi wanatetewa wa wakili Asifiwe Alinanuswe ambaye alipotakiwa kuzungumzia shtaka hilo alisema hajapewa maelekezo ya kuzungumzia kesi hiyo kutoka kwa mteja wake.
"Kwanza ningejua kuna waandishi ningeweka zuio la waandishi kupata taarifa hizi, hivyo kaandikeni mlichopata kwa wakili huyo mwingine, wateja wangu hawajanipa maelekezo ya kuzungumza nanyi," alisema.
Hakimu Mfawidhi Lukumai ameahirisha kesi hiyo baada ya upande wa utetezi kuweka pingamizi la kutaka kesi hiyo isikilizwe faragha na imepangwa kuanza kusikilizwa kwa pingamizi hilo Februari 21, 2023.
Chanzo:Jamii Forums