Mkuu wa Mkoa wa Njombe Antony Mtaka amemuagiza mkuu wa Wilaya ya Njombe Kissa Kasongwa kuwakamata na kuwafanyisha usafi kwenye mashuleni pamoja na vituo vya afya wazazi wote ambao watoto wao hawajaripoti shuleni kuanza muhula mpya wa masomo badala ya kuwaweka rumande
Mtaka ametoa agizo hilo akiwa katika shule ya Sekondari Mbeyela iliyopo mjini Njombe wakati akikagua wanafunzi walioripoti shuleni ambapo katika shule hiyo wanafunzi wa kidato cha kwanza wameripoti wanafunzi 62 pekee kati ya 300 waliopaswa kuanza masomo.
"Hatuwezi kuruhusu watu kufanya ujinga kwenye suala la elimu nikuagize mkuu wa wilaya ya Njombe kamata wazazi wote ambao hawajaleta wanafunzi shuleni beba magari ya polisi yote wapakiwe humo ili waje wafanye usafi wa vyoo na madarasa"
Mtaka amesema hakuna sababu ya kuwapeleka rumande wazazi hao wakamalize chakula Cha serikali hivyo wanapaswa kufanya usafi kwani haiwezekani serikali ikajenga madarasa na kufuta ada halafu wazazi washindwe kuwapeleka watoto shuleni.
Hata hivyo Mkuu wa shule ya Sekondari Mbeyela Mwalimu Jimmy Ngumbuke amesema kasi ya wanafunzi kuripoti shuleni ni ndogo na hivyo jitihada zaidi zinahitajika kwa wazazi.