FAMILIA ya aliyekuwa mfanyakazi wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Henry Massawe, imeingia kwenye mvutano wa wapi uzikwe mwili wa mpendwa wao huyo kwa kile kilichodaiwa wosia wa marehemu.
Mke wa marehemu, Janeth Ikuyumba anataka mwili wa mumewe ukazikwe Moshi mkoani Kilimanjaro alikozaliwa wakati ndugu wa marehemu wanataka uzikwe nyumbani kwake Kiharaka, Bagamoyo mkoani Pwani.
Licha ya kaburi kuchimbwa nyumbani kwake Kiharaka, mwili wa kijana huyo aliyefariki dunia Januari 16 mwaka huu kwenye Hospitali ya Regency jijini Dar es Salaam, haujazikwa.
Mmoja wa mashuhuda wa mgogoro huo ambaye aliomba hifadhi ya jina lake, alidai kuwa kabla ya kifo chake, kijana huyo aliyekuwa Ofisa Viwango TBS, aliomba akifariki dunia, azikwe nyumbani kwake.
"Ijumaa (iliyopita), tuliandaa kaburi ili tumzike Henry lakini mvutano ulizidi kiasi kwamba tulishindwa kuzika. Mke anadai kwamba anataka kuipangisha nyumba, hivyo kukiwa na kaburi, itamkosesha biashara," alidai shuhuda huyo.
Aliendelea kudai kuwa mke amekataa kumzika mumewe kwenye eneo alilochagua kwa kuwa "hata akitaka kuuza nyumba, itakuwa ngumu kuuzika."
Alisema kuwa Masawe ameacha mtoto mmoja wa kiume anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka miwili.
NIPASHE ilipomtafuta mke wa marehemu, Janeth Ikuyumba kuhusu suala hilo, alikataa kulizungumzia kwa madai kwamba aliyetoa taarifa ya mvutano huo, anayo maelezo ya kutosha.
"Kamuulize huyo aliyekwambia hizi habari, akufafanulie zaidi maana inaonekana anajua kila kitu, mimi sina cha kusema," alisema.
NIPASHE ilimtafuta dada wa marehemu, Sesilia Massawe ambaye alithibitisha kuwapo mvutano huo.
Hata hivyo, alishindwa kutoa ufafanuzi zaidi kwa maelezo kuwa yuko kikaoni na kwa zaidi ya saa tatu alikuwa kikaoni na kila akipigiwa alijibu kuwa hawezi kuongea kwa kuwa kikao kilikuwa hakijamalizika.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kiharaka Magengeni, Simon Kilian alithibitisha kuwapo mvutano huo, lakini alikataa kutoa ufafanuzi kwa njia ya simu.
Jirani wa familia hiyo, Fatuma Chombo, alidai: "Tumeishi na Henry vizuri sana, alikuwa anasalimia mkubwa hadi mdogo, kaburi limeshachimbwa halafu tunaambiwa hatazikwa Kiharaka, tupo hapa hadi azikwe hapa.
"Tunasikia mke anataka asafirishwe lakini ndugu wa mume wanataka azikwe hapa, jana (juzi) tulikuwa hapa tukatangaziwa anazikwa leo (jana), cha ajabu tumefika hapa tunaambiwa hazikwi hapa na kaburi limechimbwa."
Alidai kuwa awali waliambiwa hawawezi kuchimba kaburi hadi kibali kipatikane na walitafuta kibali kikapatikana kwa viongozi wote na kuruhusiwa kuchimba kaburi tangu juzi.
Alidai kuwa kijana huyo alitakiwa kuzikwa Januari 20, mwaka huu, lakini hadi jana mwili ulikuwa haujafika nyumbani.
Chanzo: Nipashe