Mkuu wa wilaya ya Butiama mkoani Mara Moses Kaegele amekanusha kauli inayotajwa kutolewa na mkuu wa mkoa huo kwamba wanafunzi wa kike watakaguliwa ili kubaini kama wamefanyiwa vitendo vya ukeketaji, kwenye mkutano uliohusisha wadau wa huduma na maendeleo ya jamii.
Hayo yanajiri baada ya Mbunge wa viti maalumu Neema Lugangira kuhoji juu ya suala hilo baada ya kuona likiripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari na kueleza kuwa suala hilo ni ukatili wa kijinsia na ni kinyume na haki za watoto.
"Nimesoma taarifa inaeleza kuwa mkuu wa mkoa wa Mara ameelekeza mkoa huu unatarajia kuweka taratibu ya kuwakagua Wanafunzi wa kike kama wamekeketwa au la, nataka kufahamu hili suala litatekelezwaje kwa sababu hili suala sio sahihi," Alisema Mbunge Neema Lugangira.
Kwa upande wake muwakilishi wa mkuu wa mkoa wa Mara, Mkuu wa Wilaya ya Butiama ameeleza kuwa mkoa huo hauna mpango wa kutekeleza suala hilo kwani hadi sasa hakuna taarifa yoyote inayozitaka shule kufanya hivyo na kuwaomba wadau na wabunge kutumia majukwaa yao kukemea vitendo vya kikatili hususani ukeketaji kwani imekua changamoto kubwa mkoni Mara.
"Mkoa wa Mara ni miongoni mwa mikoa ambayo ukeketaji umekithiri na Mkuu wa Mkoa amekua akipambana sana, Lakini nawahakikishia kwamba hakuna waraka wowote ambao unaagiza shule kukagua wanafunzi kwasababu sisi kama mkoa tunaheshimu sheria za nchi labda tuwaombe wabunge muendelee kulipigia kelele suala hili bungeni," Ameeleza mkuu wa Wilaya Moses Kaegele.