Waziri wa Kilimo Hussein Bashe ameagiza Kampuni ya Kandia Fresh ya Mkoani Njombe ifungiwe kujihusisha na ununuzi/uuzaji wa matunda aina ya parachichi na kukamatwa kwa Mmiliki wake kwa sababu Kampuni hiyo ilinunua maparachichi ambayo hayajakomaa na kuyamwaga kwenye dampo la Maheve Halmashauri ya Mji wa Njombe.
Bashe ametoa agizo hilo baada ya kukagua nyumba ya kuhifadhi na kufungasha matunda na mbogamboga mjini Njombe wakati alipofanya ziara Mkoani humo ambapo alielekezea kusikitishwa kwake na kitendo cha Mnunuzi David Baraza kuyamwaga matunda hayo na kuzua taharuki baada ya video fupi kusambaa mitandaoni.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Njombe Kissa Kasongwa amesema kwa mujibu wa maelezo ya Afisa Kilimo wa Halmashauri ya Mji wa Njombe Watu waliovuna parachichi hizo walikamatwa kwa makosa mawili ya kukwepa ushuru na kununua parachichi bila ya kibali wakiwa na tani 11.5 ya maparachichi ambayo ni madogo na hayajakidhi soko.