Jeshi la Polisi mkoani Mtwara linamshikilia dereva wa bodaboda, mkazi wa Kijiji cha Naipanga wilayani Nachingwea mkoani Lindi kwa tuhuma za mauaji ya mwanamke mmoja aitwaye Mwajuma Tufani (32) baada ya kumpiga na nondo pamoja na mawe kichwani na kisha kuutelekeza mwili wake kando mwa barabara iendayo Nachingwea kutokea Masasi.
Taarifa iliyotolewa na Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Mtwara, ACP Nicodemus Katembo imeeleza kuwa tukio hilo limetokea usiku wa Januari 4 mwaka huu.
ACP Katembo amesema chanzo cha mauaji hayo ni kwamba, marehemu alimkabidhi mtuhumiwa fedha taslimu kiasi cha shilingi 300,000 ili akanununue korosho kwa makubaliano kuwa ataziuza na kupata faida ya shilingi 500,000, lakini baadaye mtuhumiwa huyo alimtumia marehemu shilingi 40,000 pekee badala ya shilingi 500,000, kama walivyokubaliana.
Aidha, ameeleza kuwa kutokana na kutotimiza ahadi, marehemu alimtaka mtuhumiwa waende sehemu zote ambazo alipeleka korosho hizo ili kujiridhisha, na wakati wakiwa njia kuelekea maeneo hayo aliyokuwa anadai, mtuhumiwa alijifanya pikipiki imeishiwa mafuta na marehemu aliposhuka kwenye chombo ndipo alianza kumshambulia kwa nondo na mawe hadi alipofariki dunia.