Mwanaume mmoja aliyefahamika kwa jina la Emmanuel Sanga mkazi wa Wilaya ya Kyela mkoani Mbeya anatuhumiwa na serikali ya kijiji cha Katumba Songwe kwa kosa la kumuunguza mzazi mwenzie (Scola Mpela) kwa maji ya moto.
Akizungumzia tukio hilo mtendaji wa kijiji cha Katumba Songwe Lusajo Mwakapiso amesema alipata taarifa ya tukio hilo siku ya ijumaa tarehe 13.01.2023 majira ya saa 2 usiku ndipo alipoamua kutuma watu kwaajili ya kumkamata muhusika ambaye alikamatwa majira ya saa 7 usiku.
Ameeleza chanzo cha tukio hilo ni kuwa mwanaume huyo alifika katika makazi ya mzazi mwenzie na kumshutumu kuwa na mahusiano na mwanaume mwengine jambo ambalo lilileta mzozo baina yao na mwanaume kupiga teke maji ya moto yaliyokuwa jikoni na kumuunguza Scola.
Akizungumza mbele ya kamati ya ulinzi na usalama ya kijiji, mtuhumiwa alikiri kosa na kuomba kusamehewa kwani alikuwa hajitambui wakati anafanya jambo hilo, lakini msamaha huo haukuwa chochote kwani mara baada ya kamati ya ulinzi na usalama ya kijiji kusikiliza pande zote mbili za wahusika ilitoa maamuzi ya kesi hiyo kufikishwa kituo cha polisi kwa ajili ya sheria kufuata mkondo wake.
Muathirika amepatiwa matibabu katika zahanati ya kijiji cha Katumba Songwe mpaka sasa hali yake inaendelea vizuri.