Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba ametoa ufafanuzi kuhusu kiwango cha deni la Taifa ambalo hujengwa kwa kujumlisha deni la Serikali kuu, deni la sekta binafsi pamoja na amana za Serikali (bills na bonds).
Dkt. Nchemba ametoa ufafanuzi kufuatia taarifa kuhusu deni la Taifa kufikia TZS trilioni 91 hadi Oktoba 22, jambo lililoibua mjadala mkubwa mitandaoni huku baadhi ya wananchi wakiikosoa Serikali kwa kile walichodai kuwa inakopa sana.
Katika ufafanuzi wake, Dkt. Nchemba ameonesha kuwa deni la Serikali kuu ni USD bilioni 201.1 (TZS trilioni 46.6), na deni katika amana za Serikali ni TZS trilioni 26.6 hivyo kufanya jumla ya deni la Serikali kuwa TZS trilioni 73.2
Aidha, amesema deni la Taifa kama ilivyoripotiwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) limepanda hadi kufikia 91 kwa sababu ya kuongezeka kwa deni la sekta binafsi ambapo kampuni za Kitanzania zimekopa USD bilioni 7.3 (TZS trilioni 17) siku za karibuni.
Hata hivyo amesema ni kawaida kwa kampuni binafsi kukopa kwani ndio njia yao ya kupata mitaji.
“Yanawekeza kwa kukopa, sekta binafsi inakua kwa kukopa, hivyo hii hata sio jambo la kushtua,” ameeleza huku akiongeza kuwa “tunatoa rai makampuni binafsi yaendelee kukuza mitaji na kuwekeza.”
Kwa mujibu wa Bajeti ya Serikali mwaka 2022/23, tathmini ya uhimilivu wa deni la Serikali uliofanyika Novemba 2021 ulionesha kuwa viashiria vya deni la Serikali viko ndani wigo unaokubali kimataifa katika kipindi cha muda mfupi, wa kati na mrefu.