Mamia ya wananchi wamejitokeza kuaga miili ya wanandoa Grayson Ngogo (48) na Janeth Luvanda (42) leo Jumatano Desemba 28, 2022 jijini Mbeya.
Wanandoa hao, Ngogo ambae alikuwa mhadhiri na Makamu Mkuu wa Chuo cha St Agrey jijini Mbeya na mkewe Janeth aliyekuwa mwalimu wa Shule ya Sekondari ya Lejiko ni miongoni mwa watu watano waliofariki dunia katika ajali iliyotokea katika eneo la Iyovi mkoani Morogoro Desemba 25.
Akizungumza wakati wa kuaga miili hiyo leo Jumatano Desemba 28, 2022, Spika wa Bunge Dk Tulia Ackson amesema kuwa wanalia kwa sababu wawili hao hawakujua kama watapoteza maisha.
“Hakuna aliyejua kama wapendwa wetu wangepoteza maisha, hata neno la Mungu limesema pamoja na kupumzika katika tabu sisi tunaokufa katika bwana matendo yetu yataambatana nasi”amesema.
Amesema kutokana na tukio hilo la kusikitisha lililo wakutanisha, jamii inapaswa kumrudia Mungu kwa kutenda matendo yaliyo mema.
Dk Tulia amesema katika kipindi hiki cha mwisho wa mwaka hususan mkoa wa Mbeya zimejitokesa ajali na misiba mingi iliyogharimu maisha ya Watanzania.