Watu wawili, akiwamo mjamzito, wamefariki dunia na wengine wawili kujeruhiwa katika Kata ya Mahembe wilayani Kigoma baada ya kugongwa na pikipiki wakati wanakamata kumbikumbi pembezoni mwa barabara iendayo Gereza la Kwitanga karibu na Mto Kaseke.
Tukio hilo limetokea karibu na eneo la kichuguu ambacho wakazi wa eneo hilo hukamata kumbikumbi kila msimu wa masika unapoanza.
Akizungumza na waandishi wa habari juzi, Kamanda wa Polisi mkoani Kigoma, Filemon Makungu alisema vifo hivyo vya Neema Moshi (18) na Sia Ramadhan (20) vilisababishwa na dereva anayejulikana kwa jina la Yeovan Kagizo (28), akiwa anaendesha pikipiki yenye namba za usajili MC 602 CPJ kwa mwendo mkali, alishindwa kuimudu na kusababisha ajali iliyosababisha vifo.
"Tukio hilo liliripotiwa Novemba 30, 2022 majira ya saa sita mchana ambapo dereva huyo alishindwa kupishana na bodaboda mwenzake katika barabara ya Mahembe - Kwitanga kwa sababu alikuwa katika mwendo kasi na kuwagonga wanawake wawili miongoni mwa wengi waliokuwa pembezoni mwa barabara wakifanya shughuli zao za kuokota kumbikumbi na kusababisha ajali na kisha kufariki dunia walipokuwa wakipata matibabu katika Kituo cha Afya cha Bitale," alisema.
Kamanda Makungu alisema Jeshi la Polisi linamshikilia dereva huyo kwa hatua zaidi na kutoa rai kwa madereva bodaboda kuendesha kwa kufuata taratibu na kanuni za usalama barabarani na kuzingatia mwendo unaokubalika kwenye makazi ili wadhibiti pikipiki zao na kuepusha ajali.
Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa Mtaa wa Mgawa, Kijiji cha Mahembe Kati, Simon Daniel alisema wamesikitishwa na tukio hilo ambalo ni la pili kutokea eneo hilo kwa ajali zitokanazo na vyombo vya moto, likitanguliwa na la mwaka 2020 ambalo mwanamke mmoja aliyekuwa anakwenda sokoni kuuza nyanya, aligongwa na gari na kupoteza maisha.
"Sasa ajali imewachukua wengine wawili huku mmoja wao (Neema Moshi) akiwa na ujauzito wa takribani miezi mitano, inatuumiza sana, ninawaomba wananchi tuwe makini tunapotembea barabarani kuepusha ajali," alisema.
Shuhuda wa tukio hilo ambaye pia alipata majeraha kwenye mguu kutokana na ajali hiyo, Salma Stephano alisema: "Kama ilivyo kawaida kwa kichuguu hicho kutoa kumbikumbi kila mwaka, siku hiyo pia kilitoa kumbikumbi ambapo wengi wao walikusanyika katika eneo hilo la Kaseke pembezoni mwa barabara kilipo kichuguu na kukizunguka huku tukiendelea kuwakamata kwa lengo la kuwala na biashara, ghafla tulipoo pikipiki ikitufuata kwa kasi na kisha nikapoteza fahamu.
"Nilipopata fahamu kulikuwa na mtu mmoja amechomwa na chuma kwenye mguu kama mimi, mwingine amelaliwa na pikipiki, baadaye nikaona wengine wawili wamelala chini wakiwa wanapepewa, nilisaidiana nao, baada ya muda walichukuliwa na bodaboda na kupelekwa Kituo cha Afya Bitale, haikupita muda mrefu tukaambiwa wamefariki (dunia)."
Tamasha Bahati, mkazi wa Mahembe, alisema kumbikumbi hutumika kama mboga na mara nyingi hupatikana siku moja tu ya msimu wa mvua kuanzia majira ya saa tatu asubuhi mpaka majira ya jioni na hivyo wengi wao hasa kinamama na watoto huacha kazi siku hiyo kwenda kukamata kumbikumbi.
Alisema siku hiyo ya tukio, alikuwapo eneo la tukio japo aliondoka kabla ya tukio, akibainisha aliwahi kuondoka ili kwenda kupika na kwamba ndani ya muda mfupi baada ya kuondoka kwenye kichuguu hicho, alisikia kelele na alipotoka kwenda kuangalia akakuta mmoja kati ya majeruhi ameshapelekwa hospitalini na baadaye akachukuliwa wa pili na baada ya nusu saa waliletewa taarifa ya vifo vyao.
Chanzo: www.tanzaniaweb.com