Mwalimu atupwa jela miaka 20


MAHAKAMA ya Wilaya ya Mufindi imemhukumu kifungo cha miaka 20 jela Jalio Mtanga (53) ambaye ni mwalimu wa Shule ya Msingi Nyololo baada ya kutiwa hatiani kwa makosa saba ya ukatili mkubwa wa kijinsia aliowafanyia wanafunzi saba wa shule hiyo.


Mwalimu huyo amehukumiwa baada ya ushahidi kuthibitisha kufanya kosa la ukatili mkubwa wa kijinsia ambalo ni kinyume cha kifungu cha 138 C cha Sheria ya Kanuni za Adhabu.

Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa mshtakiwa huyo kwa nyakati tofauti, aliwafanyia ukatili huo watoto wa shule hiyo wenye umri kati ya miaka 10 na 16 ambao alikuwa akiwarubuni kwa kuwaambia wakusanye madaftari na kisha kupeleka ofisini kwake ambako ndiko alikuwa akitekeleza unyama huo.

Wakili wa Serikali Twide Mangula baada ya mshtakiwa kutiwa hatiani, aliiomba mahakama hiyo itoe adhabu kali kutokana na kukithiri kwa vitendo hivyo huku waathirika wakubwa wa vitendo hivyo wakiwa watoto wa kike.

Akisoma hukumu, Hakimu Mkazi Mwandamizi, Benedict Nkomola alisema  kutokana na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo, Mtanga anastahili kifungo hicho ili iwe fundisho kwake na jamii kwa ujumla.

Mshtakiwa alipopewa nafasi ya kujitetea, aliiomba mahakama impunguzie adhabu kwa kuwa ana familia inayomtegemea.

Hata hivyo, mahakama ilitupilia mbali maombi hayo na kumhukumu kutumikia kifungo hicho jela.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo