Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Antony Sanga akizungumza alipofanya ziara ya kikazi katika kata ya Mlondwe.
Na Edwin Moshi, Makete
Serikali imesema itatoa kiasi cha shilingi milioni 100 kwa ajili ya kutatua
tatizo la maji Mlondwe wilayani Makete mkoani Njombe ambalo limepelekea kero
kwa wananchi wa eneo hilo
Akizungumza baada ya kufanya ziara ya kikazi kijijini hapo Katibu Mkuu wa
Wizara ya Maji Mhandisi Antony Sanga baada ya kujionea changamoto za mradi huo
amesema serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan
haina shida ya fedha hivyo kwa kuwa eneo hilo lina shida ya maji amewasiliana
na Waziri wa maji Jumaa Aweso, kabla ya wiki hii kumalizika serikali itawaletea
shilingi milioni 100 kwa ajili ya kutatua changamoto ya maji
Katibu Mkuu Sanga amemuagiza Meneja wa RUWASA wilaya ya Makete Mhandisi
Innocent Lyamuya kujipanga kupokea fedha hiyo kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa
maji Mlondwe ili kuondoa changamoto hiyo huku akihimiza mradi huo ujengwe kwa
kasi ili ukamilike kwa wakati na wananchi waanze kupata huduma ya maji
"Hata huu mradi muujenge kwa kasi, haya matenki muendelee nayo lakini
wakati huo yale mabomba m-diverge (myachepushe)wananchi wapate maji, kwa hiyo
ndugu zangu kina mama wa Mlondwe, waheshimiwa viongozi wote wa Mlondwe,ndugu
zangu wananchi wenzangu wa Mlondwe wiki ijayo (wiki hii) tunawaletea fedha
mtakapoombwa ushirikiano basi muwe tayari ili ndani ya muda mfupi basi muanze
kujenga mradi huu wa maji ambao mmechukua muda mrefu ninyi kunufaika nao"
amesema Mhandisi Sanga
Awali Meneja wa RUWASA wilaya ya Makete Mhandisi Innocent Lyamuya akitoa
taarifa kwa Katibu Mkuu ya Mradi wa Maji Mlondwe amesema mradi huo ulitegemewa
kugharimu shilingi Bilioni 2 na milioni 84 na mpaka sasa umegharimu shilingi
Bilioni 1.5 ambapo amesema walipokuwa wanaingiza maji kwa watu, mabomba
yaliyopo kwa kuwa ni ya zamani yalishindwa kuhimili na yapasuka hali
iliyochangia kuwepo na upotevu wa maji
"Sasa hii imechangia kuwepo na changamoto ya upotevu wa maji pamoja na
kwamba mradi umeleta maji ya kutosha sasa kuna upotevu wa maji mengi huku
njiani kutokana na ile miundombinu kuwa ya zamani hivyo hiyo ni changamoto
kubwa ya huo mradi" - Amesema Mhandisi Lyamuya
Amesema kwa kuwa mradi huo una bakaa ambayo imebaki na kwamba
wameshafanikisha maeneo mengi wanaomba kwamba kwenye njia za usambazaji waweze
kupatiwa fedha ili waweze kumalizia sehemu zilizobaki ikiwemo kubadilisha
mabomba ya zamani na kuweka mabomba mapya ili wananchi wapate maji kwenye
maeneo yao
"Mh Katibu Mkuu kwa kifupi sana hiyo ndiyo taarifa ya huu mradi ni
mradi mzuri sana na umetekelezwa vizuri matenki makubwa lakini changamoto
iliyopo mkuu ni hiyo kwenye maeneo ya njia za usambazaji" amesema Meneja
huyo wa RUWASA
Naye Mwenyekiti wa Chama cha mapinduzi (CCM) Wilaya ya Makete Clemence
Ngajilo amesema wao kama chama walifaya ziara na kujionea changamoto ya maji inayowakabili
na kuahidi kulishughulikia hivyo ujio wa Katibu Mkuu huyo ni ishara tosha
kwamba serikali inawajali wananchi wake
Diwani wa kata ya Mlondwe Alphonce Salimo ameshukuru kwa hatua hizo
zilizochukuliwa na serikali na kukiri kuwa walikuwa wakisumbuliwa na mvujo wa
maji hivyo wanaimani kwamba tatizo hilo litakwenda kumalizika huku mmoja wa
wakazi wa kijiji hicho akishukuru kwa hatua hizo ambazo zitawapunguzia adha ya
kutembea umbali mrefu kutafuta huduma ya maji.