Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan akibonyeza kitufe maalum kuashiria kuanza kwa zoezi la kujaza maji katika mradi wa Bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere lililopo Rufiji, Mkoani Pwani
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan amewaagiza wakuu wa mikoa nchini kutekeleza maagizo aliyoyatoa Makamu wa Rais Dr Philip Mpango hivi karibuni ya kuhakikisha kwamba mifugo yote ambayo imeingia katikka bonde la mto Rufiji kinyume na utaratibu inaondolewa
Rais Samia ametoa kauli hiyo ya msisitizo wakati akizungumza kwenye zoezi la uzinduzi wa tukio la kuanza kujaza maji Kwenye Bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere lililopo Rufiji, Mkoani Pwani leo tarehe 22 Desemba, 2022
Katika hotuba yake Rais Samia aameagiza pia kuwa Wananchi, Wafanyabiashara, na taasisi zote ambazo zinachepusha maji katika maeneo mbalimbali hasa bonde la mto rugiji wazuiwe mara moja ili maji yote yarejeshwe katika mkondo wake wa asili
"Nisitize uzingatiaji wa maelekezo ya Makamu wa Rais aliyotoa juzi, kwamba mifugo yote ambayo imeingia kwenye bonde hili kinyume na utaratibu iondolewe, wakuu wa mikoa mpo hapa, kwa mifugo itakayohamia kwenye vijiji katika bonde uwezo wa vijiji uangaliwe sio tu kumimina mifugo"
"Wananchi na wafanyabiashara na taasisi zote ambao wanachepusha maji katika maeneo mbalimbali hasa bonde la mto Rufiji wazuiwe, ili maji yote yarejeshwe katika mkondo wake wa asili" amesema Rais Samia
Aidha akizungumzia historia ya bwawa hilo Rais Samia amesema kuwa mafanikio makubwa yaliyopatikana ni kutokana na fikra za baba wa Taifa la Tanzania Mwalimu Nyerere na utekelezaji ulioanzia kwa Rais wa awamu ya Tano Dkt John Pombe Magufuli ambapo amewataka watanzania kuwaombea viongozi hao
Awali akimkaribisha Rais Samia, Waziri wa Nishati January Makamba amesema kuwa mpaka sasa serikali ya Tanzania haidaiwi na mkandarasi wa mradi huo kwani serikali imekuwa ikilipa kwa wakati katika kila hatua ya mradi huo
"Mradi huu ni wa fedha nyingi na kwa mujibu wa mkataba pale fedha zinapochelewa kutolewa kwa malipo ya kila hatua inayofikiwa huwa kuna adhabu, Mheshimiwa Rais hatujawahi kuchelewa hata mara moja katika mara zote ambazo tumefanya malipo na hadi leo hatudaiwi hata senti moja"
Kwa upande wake mkurugenzi mkuu wa TANESCO, Maharage Chande amesema kuwa mradi huo umeajiri watu 12,275 hadi kufikia mwezi Novemba ambapo kati ya wafanyakazi hao waajiriwa watanzania ni 11164 sawa na asilimia 90.97 na wafanyakazi kutoka nje ni 1111 sawa na asilimia 9.1"
"Mradi huu unakadiriwa kutumia trilioni 6.5 na mpaka mwisho wa mwezi Novemba serikali imemlipa mkandarasi trilioni 4.5 ambayo ni kama asilimia 70 za mradi, fedha za mradi huu ni fedha za kodi zetu watanzania"
"Mradi huu umeajiri watu 12,275 hadi kufikia mwezi Novemba, kati ya wafanyakazi hao waajiriwa watanzania ni 11164 sawa na asilimia 90.97 na wafanyakazi kutoka nje ni 1111 sawa na asilimia 9.1"
Mradi huo wa Kufua Umeme wa Bwawa la Mwalimu Julius Nyerere (JNHPP) umekamilika kwa asilimia 78.68 na unakadiriwa kutumia trilioni 6.5 ambapo ukikamilika utazalisha megawati 2,115 zitakazoongeza nguvu katika megawati 1,500 zinazozalishwa na vyanzo mbalimbali vya sasa na kuondoa tatizo la uhaba wa umeme nchini.