Sintofahamu maiti 19 kukosa ndugu Dodoma

Wakati baadhi ya watu wakiripotiwa kupotea, chumba cha kuhifadhia maiti Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma kina miili 19 iliyokosa ndugu, huku 12 ikizikwa na Halmashauri ya Jiji baada ya kupokewa zaidi ya miezi miwili iliyopita.


Sakata la miili hiyo liliibuliwa baada ya mwili wa kijana mwenye miaka 25 hadi 30 kuokotwa kwenye kiroba Desemba 5 mwaka huu, jirani na Shule ya Jamhuri.

Mhudumu wa chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitalini hapo, Beda Anthony alisema miili hiyo haikuwa na ndugu hivyo utaratibu wao ni kukabidhi jiji ambao huizika.

Beda alisema kumekuwa na utaratibu wa kisheria kwamba mwili ukikaa hapo kwa siku 14 bila kutambuliwa, Halmashauri ya Jiji hukabidhiwa kwa taratibu za mazishi na ndicho kilichofanyika.

Alisema sehemu kubwa ya miili hiyo ni vijana wa kiume wenye umri wa kati ya miaka 25 hadi 35, lakini wengi huwa na majeraha kichwani.

“Ule wa kiroba nao umezikwa, baada ya kukaa nao wiki mbili, taratibu zinatutaka kukaa na mwili siku 14 lakini wakati mwingine huwa tunaongeza siku tukiamini ndugu wanaweza kujitokeza,” alisema Beda.

Kauli ya mhudumu huyo inaungwa mkono na mganga mfawidhi wa hospitali hiyo, Ernest Ibenzi ambaye alisema ni utaratibu wa kawaida kupokea miili na kuihifadhi.

“Huwa tunapokea miili hii kutoka kwa wenzetu polisi, lakini muda ukifika tunawapa taarifa watu wa jiji ambao huja kuichukua kwa ajili ya kwenda kuwahifadhi katika nyumba zao za milele,” alisema Ibenzi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Martin Otieno alisema huwa wanapokea taarifa za vifo au majeruhi na kuwapeleka hospitali.

“Inapokuwa imekosa ndugu hilo si jukumu letu, wanaopaswa kuulizwa hapo ni wenzetu wa upande huo au mamlaka za Jiji,” alisema Otieno.

Mmoja wa watumishi wa jiji ambaye aliomba jina lake kuhifadhiwa, alisema huwa wanakwenda kuichukua miili na kuizika kwa taratibu za kiserikali.

Hali kama hiyo imeshuhudiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya, Mganga Mfawidhi Abdallah Mmbaga alisema kwa mwaka huu watu wawili walifariki dunia wakati wakiendelea kupatiwa matibabu baada ya kutelekezwa na ndugu zao.

Dk Mmbanga alisema wagonjwa hao wameripotiwa kwa kipindi cha Januari mpaka Desemba mwaka huu na miili yao ilikabidhiwa jiji kwa taratibu za mazishi.

Sheikh wa Mkoa wa Dodoma, Mustapha Rajabu alisema jambo hilo ni kubwa na la kustusha, huku akiomba mamlaka zinazohusika kuwashirikisha viongozi wa dini ili wawaombee marehemu.

“Hata kama wanazikwa na jiji, ombi langu wahifadhiwe kwa utaratibu wasizikwe kwa kutumbukizwa, hawa ni binadamu wenzetu,” alisema Sheikh Rajabu.

Askofu Mkuu wa Kanisa la Endless Harvest (EHC) Dodoma, Elia Mauza alisema ataandaa ibada maalumu kuwaombea marehemu hao kwa kuwa hakuna ajuaye walikuwa ni wakina nani na nafasi zao kwenye nyumba za ibada.

“Hata kama hawana ndugu, sisi tuliosikia ndio ndugu zao, nitaandaa ibada maalumu Jumapili katika kanisa langu kwa ajili ya kuwaombea, lakini inasikitisha,” alisema Askofu Mauza.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Chang’ombe Juu, Mwanaisha Ramadhan alisema kumekuwa na changamoto ya baadhi ya watu kubadilisha majina pindi wanapofika ugenini, ndiyo maana wanashindwa kutambuliwa.

Wakili Elias Machibya alikiri sheria inataka mwili ukae mochwari kwa siku 14 ukisubiri ndugu, zikipita inatakiwa halmashauri kuuhifadhi kukiwa na viongozi wa dini watakaofanya maombi.

Hata hivyo, Machibya alisema sheria inaruhusu mtu kuomba kibali cha mwili ufukuliwe, lakini lazima mhusika akafungue shauri mahakamani ndipo taratibu nyingine zifuate.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo