Afisa wa polisi anayetambulika kama David Mukiri, aliyempiga risasi na kumuua mhudumu wa bodaboda mwenye umri wa miaka 28 eneo la Malindi ameripotiwa kujitia kitanzi.
Kwenye tukio lililotendeka siku ya Alhamisi, Disemba 22, Mukiri ambaye ni afisa wa Kituo cha Polisi cha Malindi Airport, aliondoka kwenye lango kuu ili kuchukua bidhaa katika duka lililoko karibu. Kwa mujibu wa ripoti iliyoonekana na TUKO.co.ke, waakti aliporejea, Mukiri alikutana na mwana bodaboda, Elvis Baya Thoya na kuanza kukorofishana kuhusu jambo ambalo halikujulikana.
Hatimaye, Mukiri alimpiga risasi Thoya mara tatu kwa kutumia bastola yake rasmi yenye nambari za kipekee yaani 'serial number' CZ807 C122350, na kumuua papo hapo.
Raia walishikwa na hamaki na kuanza kupiga mawe gari la Malindi OCS hadi kioo cha mbele cha gari hilo kikavunjwa.
Maafisa wawili Nicholas Waringa na Abubakar wa Kituo cha Malindi walipata majeraha kwenye mikono ya kulia. Mwili wa Baya umehifadhiwa katika mochari ya Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Malindi huku upasuaji wa maiti ukisubiriwa. Kufuatia tukio hilo, Mukiri alitoweka na mwili wake kupatika siku ya Ijumaa, Disemba 23, katika shamba la Malindi Airport.
Polisi wamesema kwamba Mukiri alijitoa uhai kwa kujipiga risasi kwenye sehemu ya chini ya uso wake na kisha risasi ikapitia kichwani. Mwili wake umehifadhiwa katika chumba cha maiti cha Malindi, wakati uchunguzi kuhusu mkasa huo ukiendelea.
Chanzo: TUko