Jumamosi ya Novemba 26, 2022 itabaki kuwa siku ya kumbukumbu mbaya mno kwa familia ya marehemu Injinia Byemerwa.
Hii ni baada ya kupoteza mama na watoto wawili katika ajali ya gari wakati wanatoka kwenye sherehe ya mahafali ya mtoto wao ambaye naye alifariki dunia kwenye ajali.
Katika ajali hiyo iliyotokea maeneo ya Kibamba jijini Dar waliofariki ni Immaculata Byemerwa (49) pamoja na watoto wake, Jolister Byemerwa (17), aliyekuwa anafanyiwa sherehe ya mahafali siku hiyo na Janeth Byemerwa (20), mwanafunzi aliyekuwa anasoma mwaka wa tatu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Aliyenusurika ni Albert Mrema ambaye yupo chumba cha uangalizi maalum katika Hospitali ya Mlonganzila.
Leo Alhamisi Disemba Mosi, 2022, wapendwa hao wameagwa katika Kanisa la KKKT la Tabata, Kimanga jijini Dar na itafuatiwa na mazishi huko Kibaha, Mwendapole mkoani Pwani.
Chanzo:Global TV Online