Mkuu wa Wilaya ya Makete Mhe. Juma Sweda amezindua zoezi la utoaji wa chanjo ya matone ya Polio kwa watoto walio chini ya umri wa miaka 5 katika Hospitali ya Wilaya ya Makete.
Zoezi la utoaji wa chanjo yam atone ya Polio limeanza leo Desemba 1, 2022 kote nchini na litafanyika kwa siku 4 kuanzia leo Disemba 1-4, 2022 katika vituo vyote vya kutolea huduma za Afya na kwenye maeneo yenye mikusanyiko ya watu.
Akizungumza na wazazi na walezi wa watoto waliofika kuwachanja watoto wao Hospitali ya Wilaya ya Makete Mhe. Sweda amewapongeza wazazi hao kwa mwitikio mzuri na kuwasihi kuwa mabalozi kwa wazazi wengine ambao bado watoto wao hawajapata chanjo wahakikishe wanapata huduma hiyo muhimu kwa ajili ya kulinda afya za watoto.
Mkuu huyo wa Wilaya ameongeza kuwa Polio ni ugonjwa hatari kwa afya ya mtoto na anaweza kupata ulemavu au kupoteza maisha kwa sababu tu ya kukosa Kinga.
Mratibu wa Chanjo Wilaya ya Makete Huruma Mkiramweni akiwa kwenye zoezi hilo la uzinduzi amesema watoto zaidi ya 16,000 wamepata chanjo ya polio awamu iliyopita na sasa awamu ya nne wanatarajia kuwachanja watoto zaidi ya 16,000 na kuomba ushirikiano mkubwa kutoka kwa wazazi na walezi wote.
Enestina Sanga Mkazi wa Iwawa na Mzazi wa mtoto aliyefika Hospitalini hapo kupata chanjo amesema zoezi hilo ni muhimu sana kwa wazazi kuhakikisha wanawapelekea watoto wao kwenye vituo vya kutolea huduma za Afya ili kuwalinda watoto.
Chanzo:Maketedc Instagram Page