Kisa Uchawi na faini, Mashabiki Simba na Yanga Waivaa TFF

Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji ya Ligi Kuu ya Bodi ya Ligi ‘TPLB’ imemfungia Michezo mitatu na kumtoza Faini ya Shilingi 500,000, Beki wa Kushoto wa Simba SC Gadiel Michael kufuatia kosa la kuvunja Kanuni.


Taarifa iliyotolewa na Bodi ya Ligi ‘TPLB’ imeeleza kuwa mchezaji huyo alivunja kanuni za Ligi Kuu kwa kosa la kulazimisha kuingia Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine, saa 4:25 asubuhi, siku ya mchezo dhidi ya Mbeya City uliomalizika kwa sare 1-1 kwa kile alichoeleza alitaka kukagua kiwanja.

Hata hivyo imeelezwa kuwa Gadiel Michael ambaye alikuwa ameongozana na watu kadhaa waliovalia fulana zenye nembo ya klabu ya Simba, alikatazwa kuingia Uwanjani hapo kwa muda huo na walinzi, lakini alitumia hila na kufanikiwa kuingia.

Mchezaji huyo alipoingia Uwanjani hakuonesha dalili yoyote ya kukagua eneo la kuchezea na badala yake alionekana kwenda moja kwa moja hadi eneo la katikati ya kiwanja na kumwaga vitu vyenye asili ya unga.

Wakati huo huo Kamati ya usimamizi wa Ligi (TPLB) imeitoza klabu ya Simba faini ya Sh. 1,000,000 (milioni moja) kwa kosa la baadhi ya wachezaji wake kuingia uwanjani kwa kupitia mlango usio rasmi kuelekea mchezo wa sare ya 1-1 dhidi ya Mbeya City uliofanyika kwenye uwanja wa Sokoine, Mbeya Novemba 23, 2022.

Simba walilazimisha baadhi ya wachezaji wao waruhusiwe kuingia uwanjani kupitia mlango wa kuingilia jukwaa la watu maalum na walipozuiwa na walinzi wa uwanjani (stewards), Simba walitumia nguvu kutimiza nia yao.

Katika hatua nyingine Kocha wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans SC, Nasreddine Nabi amefungiwa michezo mitatu na kutozwa faini ya Sh. 500,000 (laki tano) kwa kosa la kuwashambulia kwa maneno mwamuzi wa kati na mwamuzi wa akiba wa mchezo wa kipigo cha 2-1 cha klabu hiyo dhidi ya Ihefu FC.

Nabi aliendelea kufanya kitendo hicho hata baada ya kuonywa kwa kadi ya manjano.

Maamuzi ya adhabu dhidi ya Kocha huyo kutoka nchini Tunisia, yametangazwa na Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji ya Ligi Kuu ya Bodi ya Ligi ‘TPLB’ kupitia taarifa iliyosambazwa katika Mitandao ya Kijamii leo Ijumaa (Desemba 02).

Taarifa hiyo imeeleza kuwa Kocha Nabi amekuwa na adhabu wa kukosa michezo mitatu kwa kuzingatia kanuni 42:2 (2.1) ya Ligi Kuu ya kudhibiti makocha.

Kwa Mantiki hiyo Kocha Nabi atakosa mchezo wa Jumapili dhidi ya Tanzania Prisons utakaopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, Namungo FC ambapo Young Africans itacheza ugenini Uwanja wa Majaliwa mkoani Lindi, kisha mchezo wa Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ dhidi ya Kurugenzi FC utakaorindimba jijini Dar es salaam.

Mashabiki wa Simba na Yanga wilayani Makete mkoani Njombe hawakuwa nyuma kuzungumzia adhabu hizo, Tazama video hii



JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo