Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mkoa wa Mara, kimeiomba serikali kuangalia upya mifumo ya uendeshaji wa Shirika la Umeme (TANESCO) ili kudhibiti tatizo la umeme kukatika mara kwa mara
Mwenyekiti wa chama hicho mkoa wa Mara, Lucas Ngoto, ametoa rai hiyo na kusema mtanziko wa huduma ya umeme unaoshuhudiwa hivi sasa unapaswa kudhibitiwa haraka, ili kuepusha hasara ya kiuchumi inayoweza kurekodiwa.
"Hakuna sababu ya kukosa umeme nchi hii, vyanzo vya umeme tunavyo vya kutosha, tuna gesi ya kutosha, tuna upepo, tuna maporomoko, tulikuwa tumefika mahali tunafikiria kuuza umeme nje (ya nchi) kwa sababu umeme ulikuwa mwingi," amesema Lucas Ngoto.
Kufuatia hali hiyo amemuomba pia Rais Samia Suluhu Hassan, kuunda kikosi kazi cha wataalamu kitakachochunguza changamoto hiyo, na kutoa mapendekezoa ya namna ya kuimarisha huduma ya umeme nchini, na hatimaye kuanza kuuza nishati hiyo ng'ambo ya nchi.
Hata hivyo, katika kikao chake hicho na wanahabari, kiongozi huyo amemuomba pia Waziri anayeshughulikia Mambo ya Ndani ya nchi, Mhandisi Hamad Masauni, kuweka mikakati madhubuti ya kudhibiti ajali za barabarani, zinazoripotiwa kutokea mara kwa mara na kugharimu maisha ya raia.