Mbunge wa Nzega Vijijini, Hamis Kigwangalla amesema ameuelewa ufafanuzi wa Rais Dkt. Samia kwenye hotuba yake ya jana kuhusu mabehewa na kwamba baada ya ufafanuzi wa jana anaamini yeye na wengine wameelewa.
“Wataalamu msaidieni Mama kazi, sio kila kitu mpaka aweke sawa yeye, Mimi nimekuelewa sana Mama, na nimeridhika, tusonge mbele!
“Baada ya hoja ya mabehewa kuibuka nimepata fursa ya kujifunza mambo kadhaa, ikiwemo umuhimu wa kuwa na mkakati endelevu wa mawasiliano kwa umma, kimsingi Jamii inahitaji na inastahili kupata taarifa za miradi yao; tusipowapa taarifa rasmi vizuri, wataokoteza kokote kule.
“Miradi mikubwa inahitaji communication strategy madhubuti ili kutokuacha ‘lacunae’ na hatimaye Wananchi kuishi kwa hisia na kutumia taarifa zisizo rasmi kuamini watakachoamini ama kuaminishwa, matokeo yake ni kuwalazimisha viongozi wakuu, hadi Mhe. Rais mwenyewe, kufanya kazi ya kuweka sawa baadhi ya taarifa”
“Nilipohoji kuhusu mabehewa kama ni mapya ama ya zamani, habari ilienda ‘viral’. Jamaa wengi wakanitumia clip ya mama akifafanua vizuri kabisa, kimsingi hoja yangu ikafa! nilinyamaza pamoja na wengine kuendelea kulikuza jambo hili, Watu wa TRC walizidi kupotosha na kuzalisha maswali mengi zaidi yakiwemo ya thamani ya pesa (value for money!).