Mchezaji nguli wa soka wa Brazil, Pele, kwa jina halisi Edson Arantes do Nascimento, ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 82 baada ya kuugua ugonjwa wa saratani kwa muda.
Pele alilazwa katika Hospitali ya Albert Einstein mnamo Novemba 29, ili kupokea matibabu baada kugunduliwa alikuwa na 'tumor' au uvimbe wa koloni mnamo Septemba 2021.
Mchezaji huyo alikuwa akisumbuliwa na matatizo ya figo na kibofu, kwa miaka kadhaa.
Pele aliyezaliwa 23 Oktoba 1940, amesifika kushikilia historia ya kuwa nyota wa soka duniani kwa miongo kadhaa, kwa kutinga mabao 1,281 kwenye mechi 1,363.
Mwanasoka huyo aliisaidia Brazil kunyakua kombe la dunia mnamo 1958, 1962 na hatimaye mwaka 1970. Mwaka wa 1958, aliweka rekodi ya kuwa mchezaji mchanga kushinda wote duniani, kuwahi kucheza katika fainali ya kombe la dunia akiwa na umri wa miaka 17.
Alivuma sana katika miaka ya 1970 duniani kote, hadi mwaka wa 2000 alipochaguliwa na shirikisho la mpira wa miguu duniani kuwa mchezaji bora wa karne.
Binti yake Pele, Kely Nascimento amekuwa akiwajuza mashabiki kuhusu hali ya babake kwa taarifa za mara kwa mara kwenye mitandao ya kijamii akiwa hospitalini.
Siku ya Alhamisi alichapisha picha iliyoonyesha kuwa ni mikono ya familia ya Pele kwenye mwili wake hospitalini na kuandika: "Kila kitu tulicho ni shukrani kwako. Tunakupenda sana. Pumzika kwa amani."