Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Abdulrahman Kinana amesema Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) uliopo Rufiji mkoani Pwani, ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM.
Kinana ametoa kauli hiyo leo, wakati wa sherehe ya uzinduzi wa ujazaji maji katika bwawa la kufua umeme kwenye Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) uliopo Rufiji mkoani Pwani, baada ya hatua ya kujenga tuta linalosaidia uhifadhi wa maji katika bwawa hilo kukamilika.
Rais Samia Suluhu Hassan ndiye mgeni rasmi katika hafla hiyo ya uzinduzi inayofanyika eneo la mradi, ambapo anatarajiwa kubonyeza kitufe kitakachoshusha mageti yatakayoziba njia ya mchepusho wa maji na kuruhusu maji kuanza kujaa katika bwawa.
Hatua hiyo ya kujaza maji katika bwawa hilo lenye ukubwa wa meta za ujazo 32.3, inatazamiwa kutumia misimu miwili ya mvua kukamilisha kujaa na kuruhusu kuwashwa kwa mitambo ya kufua umeme.