Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, imemfutia kesi ya mauaji mshtakiwa Maziabi Abdallah maarufu kama Mchelenga, baada ya kuridhika kuwa alikuwa na matatizo ya akili wakati anatenda kosa hilo.
Uamuzi wa kumfutia kesi hiyo imetolewa, Desemba 13, 2022 na Hakimu Mkazi Mkuu Richard Kabate, baada ya Wakili wa utetezi, Yohana Kibindu kuwasilisha mahakamani hapo ripoti ya daktari iliyothibitisha kuwa, mshtakiwa ana matatizo ya akili na kwamba hata wakati akitenda tukio hilo, alikuwa na tatizo la afya ya akili.
"Kutokana na hali hii namfutia shtaka la mauaji na kuamuru mshtakiwa huyo apelekwe Hospitali ya Isanga, Dodoma akatibiwe kwa muda wa miaka mitatu," Amesema Hakimu Kabate aliyepewa mamlaka ya nyongeza kusikiliza kesi za mauaji.