Simulizi ya mwanaume mmoja aliyefikishwa mahakamani Nairobi kwa kumuibia mpenzi wake na kumzawadia mpenzi mwingine imezua gumzo kali miongoni mwa Wakenya.
Kulingana na blogu za Kenya, Ryan Lusalishi anadaiwa kumuibia mpenzi wake kipakatalishi na viatu mnamo Novemba mwaka huu.
Anadaiwa kuchukua viatu hivyo na kumpa mpenzi mwingine kama zawadi. Kipakatalishi hicho kilikadiriwa kuwa cha bei ya elfu 25 na mpenzi huyo aliyeibiwa kwa jina Elizabeth Okumu alirejea nyumbani na kupata baadhi ya vitu vyake havipo.
“Lusalishi pia anakabiliwa na shtaka la ziada la kusafirisha mali inayodhaniwa kuwa ni ya wizi kinyume na kifungu cha 323 cha kanuni ya adhabu ambapo anadaiwa kuwa na begi na viatu vinavyosadikiwa kuwa viliibiwa au kupatikana kwa njia isiyo halali wakati anakamatwa,” Nation walisema.
Mwanaume huyo alifikishwa katika mahakama ya Makadara jijini Nairobi.
Mpenzi mwingine wa Lusalishi aliwaambia polisi wakati wa uchunguzi kwamba alirudi nyumbani na vitu hivyo na kumpa viatu ambavyo havikuwa vyema kwake.
Alikamatwa na begi na viatu vilipatikana nyumbani kwake.
Katika kesi hiyo iliyozua vichekesho mitandaoni, mwanaume huyo Aliachiliwa kwa dhamana ya Sh50, 000 na dhamana mbadala ya pesa taslimu Sh30, 000. Kesi hiyo itatajwa Januari 31, 2023, mwakani kabla ya kuanza kusikilizwa Mei 22, mwaka huo huo.