Shirika la Reli Tanzania (TRC) limesema mabehewa yote yaliyoainishwa kuletwa kwa ajili ya treni ya Reli ya Kisasa (SGR) yatakuja na kwamba yaliyoanza kuingia nchini ni ya safari ndefu.
Wiki hii katika mitandao ya jamii kumekuwa na picha zikionyesha mabehewa yaliyoletwa sio yale yaliyoahidiwa kuletwa nchini kutokana na tofauti ya muonekano wake.
Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Masanja Kadogosa amezungumza hayo leo Novemba 24, 2022 wakati Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipotembelea ujenzi wa SGR katika eneo la Kikuyu jijini hapa.
“Tayari tumeanza kupokea mabehewa 14 ya abiria kwa ajili ya uendeshaji wa kipande cha kwanza kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro,”amesema.
Amesema picha zinazosambaa katika mitandao ya jamii zinaonyesha mabehewa hayo ambayo yatapokelewa rasmi kesho Ijumaa na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa.
Kadogosa amesema picha ya mchongoko zinazoonyeshwa katika mitandao hiyo ni za treni ambazo zitatumika kwenye safari za mda mfupi na kwamba treni hizo zitawasili Juni 2023.