MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemtia hatiani Paul Meshack (25), baada ya kukiri kumuua bila kukusudia William Lupemba, kwa madai ya kuambiwa mchafu mbele ya mwanamke aliyetajwa kwa jina la Dada Bonge.
Kabla ya mshtakiwa kufanya tukio hilo, alidai Lupemba alimkosa kumchoma na kisu Meshack mara sita bila mafanikio, ndiyo sababu iliyomfanya achukue kipande cha ubao akampiga nacho kichwani na kufariki dunia baada ya fuvu la kichwa kupasuka.
Hayo yalidaiwa jana na Wakili wa Serikali, Esther Chale, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Suzan Kihawa, wakati mshtakiwa huyo akisomewa maelekezo yake ya kosa, baada ya kukiri kumuua Lupemba bila kukusudia.
Chale alidai kuwa Oktoba 4, 2017, mshtakiwa alikuwa eneo la Vungunguti Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam.
Alidai marehemu alikuwa amekaa na dada aliyefahamika kwa jina la Dada Bonge, ndipo alifika Lupemba na kumwambia mshtakiwa anaonekana mchafu, maneno yaliyompa mshtakiwa hasira na kuanza kupigana.
Ilidaiwa kuwa katika ugomvi huo, Lupemba alichukua kisu na kujaribu kumchoma nacho mshtakiwa mara sita bila ya mafanikio ndipo mshtakiwa akachukua kipande cha mbao na kumpiga nacho marehemu kichwani na mguuni kisha akaanguka na kufariki dunia.
Alidai kuwa baada ya hapo mwili ulipelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya uchunguzi na kubainika kuwa Lupemba alifariki dunia baada ya fuvu la kichwa kupasuka kutokana na jeraha la kichwani.
Mshtakiwa alikamatwa na kufikishwa kituo kidogo cha polisi cha Pugu Mnadani na baadaye alipelekwa Kituo cha Polisi Buguruni kwa mahojiano ndipo akafikishwa mahakamani.
Baada ya Chale kumaliza kusomewa maelezo hayo, aliyakubali yote na kudai kuwa ni kweli huku akionekana akiwa na sura ya huzuni na wasiwasi na pia akilia kwa mbali huku akijifuta machozi kwa kutumia kitambaa.
Hakimu Kihawa alisema kutokana na kukiri kwake kosa, maelekezo ya awali na vielelezo alivyopokea ikiwamo ripoti ya daktari, mahakama inamtia hatiani kwa kosa la kuua bila kukusudia.
Baada ya Hakimu Kihawa kumtia hatiani, Wakili wa Serikali, Shindai, alidai hawana kumbukumbu za uhalifu wa mshtakiwa lakini, wanaiomba mahakama kutoa adhabu stahiki yenye kuleta fundisho kwa mshtakiwa na kwa jamii kwa ujumla.
"Hasa kwa kuzingatia, mshtakiwa ameondoa haki ya kuishi ya marehemu ambayo ni moja ya haki za msingi za Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania inayolindwa na Katiba, mshtakiwa alijichukulia sheria mkononi kitendo ambacho hakipaswi kufanywa kisheria," alidai.
Katika utetezi wake, Wakili wa mshtakiwa, Sarumbo aliiomba mahakama impunguzie mshtakiwa adhabu kwa sababu bado ni kijana mdogo wa miaka 25 na aliyekuwa anafanya shughuli zake za kujipatia kipato na kujikimu na familia yake.
Pia alidai kuwa mshtakiwa hakudhamiria kutenda kosa hilo bali ni katika harakati za kutaka kuokoa uhai wake baada ya baada ya kukwepa visu mara sita kutoka kwa Lupemba na katika kujihami akajikuta ameua bila kukusudia.
Hakimu Kihawa aliahirisha kesi hiyo hadi Desemba 7, mwaka huu kwa ajili ya kumsomea mshtakiwa adhabu yake.