Alipofika katika hospitali ya kaunti ndogo ya Kitengela, mwanafunzi huyo alitangazwa kuwa tayari amekata roho, kilomita moja kutoka mahali alipokuwa amedungwa kisu.
Mwanafunzi huyo aliyetambuliwa kama Jibril Abdullahi na ambaye alikuwa akiishi katika shamba la Sabaki alikuwa ameenda kwenye baa usiku kujivinjari na marafiki.
"OCS Kitengela, kikosi chake cha DCI huko Kitengela walimkimbiza hospitalini. Mwili wa marehemu ulikuwa na jeraha moja la kisu upande wa nyuma wa mkono wa kulia," ilisoma sehemu ya ripoti ya polisi.
Mwanafunzi huyo mwenye umri wa miaka 26 aliripotiwa kujihusisha katika mabishano na mwanamume asiyejulikana kuhusu mhudumu wa baa hiyo kabla ya kudungwa kisu upande wa nyuma wa mkono wa kulia.
Nation iliripoti kwamba wateja wengine katika klabu hiyo walisema kisa hicho kilitokea haraka sana hivi kwamba hakuna hata mmoja wao angeweza kuingilia kati.
Mshukiwa huyo asiyejulikana aliripotiwa kumshambulia mwanafunzi huyo kwa kuwa na uhusiano wa mapenzi na kipusa wake. Mwanamume huyo akiwa na upanga na kisu alimdunga mwanafunzi huyo wa habari akiwa ndani ya klabu hiyo.
"Mshambuliaji alisikika akidai mwanafunzi huyo alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mpenzi wake. Alimwonya kabla ya majibizano kutokea na kumchoma kisu mara moja wakiwa ndani ya baa hiyo. Mshambuliaji huyo alikuwa na kisu na panga," alisema jamaa aliyeshuhudia kisa hicho.
Chanzo: TUKO.co.ke
