MTOTO Esanto Mtewa (7) wa Kijiji cha Utilili, wilayani Ludewa mkoani Njombe, amefariki dunia baada ya kuangukiwa na ukuta wa boma la nyumba wakati akijikinga mvua.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Hamisi Issah, alisema tukio hilo limetokea Novemba 10, majira ya saa 10 jioni wakati mtoto aliporudi shule na kukuta mlango wa nyumbani kwao umefungwa na kuamua kujikinga kwenye boma hilo wakati mvua ikinyesha.
"Kulikuwa na mvua kubwa sana iliyoambatana na upepo, mtoto huyu alirudi kutoka shule na nyumbani kulikuwa hakuna watu akajisitiri kwenye ukuta wa pagale ambalo ni jirani na nyumba yao," alisema Kamanda Issah.
Alisema pagale hilo lilipigwa na upepo wa mvua na kubomoa ukuta uliomwangukia mtoto.
Kamanda alisema, wazazi waliporudi walilala mpaka asubuhi bila ya kuangalia mtoto wao yuko wapi na walipomtafuta baadaye waliona ukuta umeanguka huku mguu wa mtoto ukiwa umetokeza na kubaini ni mtoto wao.
