MBUNGE wa Buchosa, Eric Shigongo (CCM) amependekeza watumishi wa umma wasio waadilifu wachapwe viboko ili kukomesha ubadhirifu wa fedha za umma pamoja na kuwalazimisha watumishi hao kuwa waadilifu.
Aidha, amesema kama Serikali haitotaka kuwachapa viboko basi itumie sheria tano zilizopitishwa na Bunge ambazo ni pamoja na Sheria ya Takukuru, sheria ya fedha, utakatishaji fedha, manunuzi na uhujumu uchumi kuwawajibisha watumishi hao wasio waadilifu.
Shigongo ametoa mapendekezo hayo leo bungeni jijini Dodoma tarehe 5 Novemba, 2022 wakati akichangia ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa.
Amesema katika halmashauri yake ya Buchosa, ndani ya ripoti hiyo amebaini kuna ubadhirifu wa Sh milioni 94 jambo ambalo anaona aibu hasa ikizingatiwa waliokula fedha hizo bado wapo uraiani.
Amesema Tanzania inaumwa magonjwa mawili ambayo ni ukosefu wa uadilifu na uwajibikaji.
Amesema licha ya Rais Samia Suluhu Hassan kutumia muda was aa 263 angani kuelekea katika nchi mbalimbali kutafuta riziki kwa ajili ya Watanzania bado, taasisi za Serikali zinaumwa magonjwa hayo mawili.
“Ninavyozungumza unaweza kusema Tanzania ina mfumuko mkubwa wa bei lakini mfumuko wa bei Sudani ni asilimia 285, Kenya ni asilimia 6.7, Uganda ni asilimia saba na Tanzania ni asilimia 4.4. Tanzania ni nchi yenye mfumuko mdogo wa bei katika nchi za Afrika Mashariki,” amesema.
