Jela miaka minne kwa Kosa la Mauaji


MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imemhukumu kifungo cha miaka minne gerezani Ayoub Jokolo baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kumuua bila kukusudia rafiki yake Said Kombo.


Adhabu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi Mkuu, Richard Kabate, ambaye alisema amezingatia hoja zilizotolewa pande zote mbili na kumkumbusha mshtakiwa asisahau kuwa rafiki yake aliyemuua alikuwa na familia inayomtegemea.


Pia alisema familia hiyo ingependa wawe naye hadi leo na kwamba anapaswa apewe adhabu inayostahili kwa kuwa mshtakiwa alikuwa na njia nyingi za kuepuka kadhia hiyo ikiwamo kukimbia baada ya kuona wanagombana.


Alisema, sheria inatoa adhabu ya kifungo cha maisha kwa kosa la mauaji na mauaji bila kukusudia kifungo cha miaka isiyopungua 11.


"Nimezingatia muda wa miaka sita na nusu umekaa gerezani, mahakama inakuhukimu kifungo cha miaka minne jela," alisema Hakimu.


Kabla ya hukumu, Wakili wa Serikali, Grace Rwila, aliiomba mahakama itoe adhabu kali ili iwe fundisho na hasa ikizingatiwa silaha ya kisu aliyotumia na sehemu aliyomchoma marehemu.


Rwila alidai mshtakiwa huyo Juni 3, mwaka 2016, marehemu alikuwa nyumbani kwake Yombo Vituka, Temeke na ilipofika saa 3:30 usiku alitoka nje na kukutana na mshtakiwa huyo.


Ilidaiwa kwamba, wakiwa hapo waligombana na mshtakiwa alitoa kisu na kumchoma nacho Kombo (marehemu) na kisha kukimbia kusikojulikana.


Wakili huyo aliendelea kudai kwamba, Kombo alidondoka chini na kuomba msaada na watu waliokuwa eneo la karibu walimchukua na kumpeleka kituo cha polisi Makangarawe kwa ajili ya kupatiwa fomu namba 3 ya matibabu kabla ya kupelekwa Hospitali ya Temeke.


Ilidaiwa kwamba Kombo alifariki wakati akipatiwa matibabu.


Juni 9, mwaka 2016, mshtakiwa alikamatwa na alipohojiwa alikiri kutenda kosa hilo na kufunguliwa kesi hiyo.


Uchunguzi wa kitabibu ulibaini kwamba, chanzo cha umauti ilikiwa ni kuvuja kwa damu nyingi kutokana na jeraha kubwa lililokuwa chini ya tumbo.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo