Dada,kaka wahukumiwa kifungo kumshambulia mama yao mzazi


MAHAKAMA ya Wilaya ya Ilala imewahukumu kifungo cha miaka minne jela Zulfikar Safraz na dada yake, Nurin Safraz, kwa kumpiga na kumshambulia kwa matusi mazito mama yao mzazi, Maria Vazi.

Wanandugu hao walitiwa hatiani jana mbele ya Hakimu Mkazi Rehema Liana baada ya kukubaliana na hoja za rufani zilizowasilishwa na mama yao akipinga uamuzi wa Mahakama ya Mwanzo Kariakoo uliowaachia huru.

Liana, akisoma hukumu hiyo, alisema mrufani hakukubaliana na uamuzi wa kuachiwa huru washtakiwa na katika kesi hiyo ya jinai ya Septemba mwaka huu upande wa Jamhuri ulikuwa na mashahidi watatu.

Akisoma ushahidi alisema siku ya tukio maeneo ya Ilala, Mtaa wa Tanga na Utete, Zulfikar alikuta watoto wakicheza nje ya nyumba yao, aliwafukuza huku akiwatukana ndipo mama yake alipomkataza kufanya hivyo.

Alisema mshtakiwa alipokatazwa aliamua kuanza kumtukana mama yake matusi mazito, alimsukuma na kumpiga.

Hakimu Liana alisema mashahidi watatu wote walishuhudia tukio hilo la kaka na dada kumshambulia mama yao, kupigwa na kutukanwa, kulikomfanya mama huyo kuhama nyumbani kwake.

"Mahakama ya Mwanzo ilikubaliana na ushahidi wa mashahidi, ilikubali kwamba washtakiwa walimtukana mama yao, walimpiga lakini mahakama hiyo iliwaachia huru washtakiwa kwa sababu hakukuwa na PF 3," alisema Liana.

Alisema kutokana na uamuzi huo, aliukatia rufani akiwa na hoja kwamba  mahakama ilighafilika kuwaachia huru bila kuzingatia ushahidi wa upande wa Jamhuri na ushahidi wa kuona wa mashahidi watatu.

Hakimu Liana alisema mrufani alishambuliwa na watoto wake na hakuna ubishi na iko wazi katika hukumu ya Mahakama ya Mwanzo.

"Kigezo cha kutokuwepo kwa PF 3 ni hoja ambayo hakuna upande wowote ulioizungumzia. Hoja iliibuliwa na Hakimu mwenyewe akajibu," alisema Hakimu Liana.

Alisema baada ya kusikiliza rufani hiyo anakubaliana na hoja za mrufani na kuwatia hatiani washtakiwa wote wawili kwa mashtaka yanayowakabili.

Walipoulizwa kama wana makosa ya zamani ili mahakama ijue na kutoa adhabu, kaka na dada waliibuka na kuzungumza tuhuma mbalimbali dhidi ya mama yao.

Kaka: Mama huyu ameshanifunga mara tano, kila kesi mwaka mmoja mmoja na kuna kesi nyingine nilifungwa 10.

Kaka: Siku moja tumetoka disko usiku tunagonga akasema tunampigia kelele, tukalala nje, akaita polisi wakatukamata nikafungwa. Nilikuwa na mdogo wangu jela, mama anachukua kodi zetu, alibadilisha majina kwenye nyumba anadai tumekufa.

Aliendelea kudai kwamba: "Katika kesi nyingine nilifungwa miezi sita Wazo, nilipasua mawe, nilipomaliza kifungo nilirudi kama filimbi nimekonda. Kesi nyingine nasafiri akanichongea nasafirisha dawa za kulevya.

“nikakamatwa Uwanja Ndege nikafungwa miaka kumi, hajaridhika sababu sijafa, mama anarudi nyumbani saa nne usiku mpaka saa tano usiku. Yuko baba wa kambo anakula hela zetu.”

Dada; Mheshimiwa huyu mama anajifanya mnyonge hapa, hatujamkosea, yeye kila siku matusi nyumbani hakuna amani. Sasa hivi tunaamani sababu nyumbani yupo mdogo wake lakini asingekuwepo matusi na ugomvi vingekuwepo. Akirudi saa tano usiku ananikuta nimeshalala, sasa hivi tuna amani.

Mama: Niliwazaa kwa mapenzi, nikawasomesha hadi kufika hapa ni nguvu zangu lakini naishi kama mfungwa nyumbani kwangu, napigwa na kuvuliwa nguo.

Hakimu Liana alisema mahakama imezingatia hoja zilizowasilishwa na washtakiwa, itatoa adhabu ili iwe fundisho kwa watoto wengine.

"Kutokana na mashtaka yenu, mahakama inawapa adhabu. Mshtakiwa  wa kwanza Zulfikar utakwenda jela miaka minne na mshtakiwa wa pili Nurin utakwenda jela miaka mine, mnayo haki ya kukata rufani, "alisema Hakimu Liana.

Chanzo:Nipashe


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo