Wagonjwa wawili waliopelekwa katika hospitali ya Taifa Muhimbili iliyopo mkoani Dar es Salaam kwa ajili ya kupatiwa matibabu kufuatia agizo ya Rais Samia Suluhu Hassan, wameruhusiwa kurudi nyumbani baada ya kupata matibabu.
Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali ya Taifa Muhimbili Profesa Mohamed Janabi amewataja wagonjwa hao kuwa ni Helena Hungoli (60) na mtoto wake Safari Gidale (34), wakazi wa kijiji cha Imbili Juu kilichopo halmashauri ya Mji wa Babati mkoani Manyara.
Amewaambia waandishi wa habari mkoani Dar es Salaam kuwa, wagonjwa hao walifikishwa hospitalini hapo kufuatia maelekezo ya Rais ambaye alipata taarifa zao kupitia vyombo vya habari.
Profesa Janabi amesema matibabu ya wagonjwa hao yamefanyika kwa muda wa miezi miwili ambapo walikuwa wakiugua ugonjwa uliosababisha nyama kuota usoni na kwenye baadhi ya viungo vya miili yao.
“Mara tu baada ya wagonjwa hao kupokelewa Agosti 7, 2022 walianza kufanyiwa uchunguzi ambapo walibainika kusumbuliwa na ugonjwa unaojulikana kama Plexiform Neurofibromatosi." amesema Profesa Janabi na kuongeza kuwa
"Ugonjwa huu hauna tiba ya moja kwa moja isipokuwa tunatibu chochote kinachotokea kama kuondoa au kupunguza uvimbe uliozidi ili kumfanya mgonjwa aweze kuendelea na shughuli zake za maisha ikiwemo kushiriki shughuli za kijamii.”