
RAIS wa Kenya William Ruto amesema kuondolewa kwa vikwazo mbalimbali vya kibiashara kati ya nchi za Tanzania na Kenya vimesaidia kufanya wananchi wa nchi hizo kunufaika zaidi huku akieleza takwimu zinaonesha kwa sasa Watanzania wananufaika zaidi.
Akizungumza leo Oktoba 10,2022 katika Ikulu ya Dar es Salaam mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, Rais Ruto ambaye yuko nchini kwa ziara ya kikazi amesema zamani watu waliona waliona bishara kati ya Tanzania na Kenya inawafaidisha Wakenya kuliko Watanzania lakini mambo yamebadilika.
“Leo tunanunua vitu vingi zaidi kutoka Tanzania kuliko Kenya, tunanunua zaidi kutoka Tanzania ni kwasababu ya ule ushirikiano ambao umesaidia kuinua biashara kati ya nchi zetu mbili na kuondolewa kwa vile vikwazo ambavyo vilivyokuwa vinazuia bishara isifanyike kati ya Kenya na Tanzania.
“Vikwazo ambavyo vimebakia vichache Rais Samia Suluhu Hassan na mimi(Rais Ruto) tumekubaliana mawaziri wetu wakutane wakamilishe haraka na kuviondoa ili biashara ikue zaidi kwa manufaa ya Tanzania na wananchi wa Kenya tukiwa sote ni watu wa jumuiya ya Afrika Mashariki.
“Niko na imani chini ya uongozi wa Rais Samia ile kazi mlivyoanzisha na Rais Uhuru Kenyata mimi nitafuatilia ili kuhakikisha ya wafanyabiashara wetu , wakulima wetu na wale wanaofanya kazi viwandani wapate manufaa ya ushirika na urafiki kati ya nchi zetu mbili tukiwa ni wana Jumuiya ya Afrika Mashariki,”amesema Rais Ruto.
Aidha amesema wamejadili kwa kina kuhusu mradi wa bomba la gasi kutoka Mtwara kupitia Dar es Salaam hadi Mombasa na baadae Nairobi nchini Kenya, wamekubaliana na Rais Samia na Serikali zao zote mbili wale wanaohusika na sekta binafsi sasa wataharakisha.
“Tuko na Suluhu ya mambo magumu na Rais Samia amesema mimi naitwa Harakakisha , hivyo tutakuwa na Suluhu na Kuharakisha na haya mambo yote yatafanyika. Tunaweza kutumia rasilimali zetu kwa ajili ya kushughuli mbalimbali za maendeleo ya nchi zetu.
“Na hivyo kuboresha sekta ya viwanda na wananchi wetu.Serikali ya Kenya tunaahidi tunafanikisha mradi wa bomba hili katika kipindi kifupi ili tuwe na gasi ambayo tutaitumia katika kuendesha viwanda vyetu.Pia tumekubaliana na Rais Samia kuweka mikakati ya kukuza sekta ya utalii kati ya nchi zetu mbili na tuko.Tunazo rasilimali za Utalii Kenya na hapa Tanzania,”amesema .
Amefafanua Kenya kuna wanyama wanatoka Tanzania na Tanzania kuna wanyama ambao wanatoka Kenya na wala hawana vikwazo na wala hawahitaji hati ya kusafiria .Hivyo kama wanyama wanaweza kufanya mambo yao bila matatizo kwanini wao washindwe.
“Vile vikwazo ambavyo vinakwamisha utalii tunataka Mawaziri na maofisa wengine wa Serikali watusaidie kwa kufanya kazi yao ili bishara ya utalii iendelee kukua na kuwa na manufaa ya watu wa Tanzania na Kenya.”
Rais Ruto pia amesema wamezungumza na Rais Samia kuhusu mambo ya mawasiliano kupitia mpango wa kuwa na mawasiliano ya pamoja kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na wameshakubaliana na Rwanda, Tanzania ,Kenya,Sudani Kusini na Uganda kufanikisha mpango huo.
“Na hapa nataka kuipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuratibu vizuri mpango huo na sasa imebakia mambo machache tu. Watanzania na Wakenya watafanya kazi pamoja na tunaamini katika kuendeleza mawasiliano biashara zitaongezeka, udugu utaongezeka , ushirikiano utaongezeka na zetu zitafaidika.Wananchi wataweza kuwasiliana kwa njia rahisi na gharama za chini,”amesma.
Aidha Rais Ruto amesema wamekubaliana na Rais Samia kuhakikisha nchi hizo zinashirikiana kukabiliana na ugaidi na bishara haramu ya binadamu na kwamba wanataka kuhakikisha wanakomesha vitendo vyote vya uhalifu huku akieleza moja ya mkakati ni vyombo vya ulinzi na usalama kwa nchi zote mbili kuimarisha mawasiliano ya kukabiliana na matukio ya kihalifu.