Wananchi Kata ya Lupila Wilayani Makete Mkoani Njombe wamepongeza jitihada za Serikali kupitia Wizara ya Maji za kuwajengea miradi ya maji.
Diwani wa Kata ya Lupila, Ernesta Lwila amebainisha hayo Oktoba 15, 2022 mbele ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye Mahafali ya 31 ya Kidato cha Nne ya Shule ya Sekondari ya Lupila.
Lwila amesema Kata yake imepokea shilingi milioni 400 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji kwenye vijiji mbalimbali ikiwemo Ludilu, Kijyombo, Malanduku na Ukange.
Amefafanua kuwa tangu kuanzishwa kwa vijiji hivyo havijawahi kuwa na huduma ya majisafi na salama lakini hivi sasa kutokana na jitihada za Serikali hali hiyo inakwenda kuwa historia.
"Tunamshukuru sana Rais wetu Mhe. Samia Suluhu Hassan, hakika Serikali yake ni sikivu, tunakwenda kuwa na huduma ya maji ya uhakika," amesema Lwila.
Aidha, amebainisha kwamba wamepokea kiasi cha shilingi milioni 100 kwa ajili ya Mradi wa Maji kitongoji cha Makyala na mpaka sasa wananchi wanaendelea na zoezi la ufyatuaji wa tofali kwa ajili ya ujenzi wa tenki la kuhifadhia maji ili kukamilisha mradi wa huo.
"Tunaipongeza sana Wizara ya Maji pamoja na viongozi wote kwa kubwa na nzuri mnayoifanya ya kuwaboreshea wananchi huduma ya maji," amesema Lwila.
Lwila amesema wananchi wa Lupila wanajivunia matunda ya Serikali yao na wanaahidi kuipatia ushirikiano wa dhati ili miradi ikamilike kwa wakati na kwa ubora unaokubalika.