Wananchi hao wamesema zoezi hilo lilikuwa likiangazia ujenzi wa vyoo bora, uwepo wa vichanja vya vyombo na endapo vinakosekana wahusika wa nyumba hizo walikuwa wakitozwa faini ya viwango tofauti tofauti vya fedha huku wengine wakisema walitozwa faini bila kupewa risiti
Julieta Luvanda ni Katibu wa Chama cha Mapinduzi tawi la Luwumbu amesema kamati hiyo imepita nyumbani kwake kufanya ukaguzi na kukuta choo chake hakina mlango hivyo akatozwa faini ya shilingi 10,000/= lakini hakupewa risiti licha ya kumdai mtendaji akajibiwa kwamba kitabu cha risiti kimekwisha hivyo awe na subira atapewa risiti yake
Mkazi mwingine wa kijiji hicho ambaye hakutaja jina lake ameelezea jinsi bibi yake alivyopigwa kofi na mtendaji wa kata na mwenyekiti wa kijiji hicho
Akiwa kwenye mkutano huo diwani huyo amepokea malalamiko ya wananchi wakidai kutozwa faini bila kupewa risiti hivyo kusema malalamiko yao ameyachukua na atayapeleka kwa malaka za juu ikiwemo kwa Mkuu wa wilaya ili hatua zaidi zichukuliwe kwa waliohusika kwa kuwa zoezi la ukaguaji mazingira sio kosa, isipokuwa hakubaliani na utaratibu uliotumika wakati wa uendeshaji wa zoezi hilo
Mwenyekiti wa kijiji hicho Sesta Kyando amesema katika utekelezaji wa zoezi hilo yeye yupo chini ya Afisa mtendaji wa Kata na kumtuhumu kuwa ni kweli alikuwa anatumia nguvu hali iliyomfanya kuendesha majadiliano naye na kumsihi kuacha kutumia nguvu kwa kusukuma watu na kubomoa vichanja ambapo mtendaji huyo alimsikiliza na akaacha
Mwenyekiti huyo amesema tuhuma zinazoelekezwa kwake kwamba naye aliwapiga wananchi wakati wa zoezi hilo sio za kweli kwa kuwa yeye hakuwepo kwenye zoezi hilo kama mshiriki bali alikuwa mtazamaji na kwa kuwa kutakuwa na mkutano na Mkuu wa wilaya mwananchi anayedai kuwa alimpiga anamruhusu ajitokeze kulisema hilo
Afisa Mtendaji wa Kata ya Luwumbu Lavenda Nyagori akizungumza Kupitia kituo cha redio Green FM amesema si kweli kwamba kulikuwa na uonevu bali zoezi hilo liliendeshwa kwa haki kwa kuwa vijiji vitatu vya kata yake ambavyo ni Luwumbu, Uganga na Usililo vimeingizwa katika mashindano ya kitaifa ya masuala ya mazingira hivyo kwa kuwa elimu imekwishatolewa, sasa ni wakati wa utekelezaji na ndiyo maana wanafanya ukazugi
Kuhusu madai ya wananchi kutozwa faini pasipo kupewa risiti, Mtendaji huyo amesema baada ya kuona vitabu vya risiti viliisha walishauriana kuorodhesha majina ya wote waliolipa faini kwa ajili ya kuja kupewa risiti zao na kwa sasa zoezi la kuwapa risiti linaendelea baada ya vitabu vingine kufika
Mtendaji Nyagori amesema zoezi hilo la ukaguzi wa mazingira litaendelea tena Oktoba 28, 2022 na kwa yeyote atakayekutwa na dosari wembe ni ule ule hivyo kutoa wito kwa wananchi kujiandaa na kutekeleza kwa vitendo elimu ya usafi wa mazingira waliyopatiwa.