Watendaji wa Kata zote 23 za Wilaya ya Makete mkoani Njombe wamesaini Mkataba wa lishe ngazi ya Jamii katika Kata zao mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Makete Mhe. Juma Sweda.
Mkataba huo umesainiwa leo Oktoba 2022 katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya Makete kwa lengo la kupambana na Utapiamlo kwa watoto chini ya miaka mitano (5).
Mkuu wa Wilaya ya Makete Mhe. Juma Sweda amewaagiza watendaji wa Kata kuhakikisha wanasimamia shughuli za Lishe kwa watoto kwenye Kata zao ili kuwa na watoto wenye Afya bora kwa kuwa Wilaya ya Makete inakubali mazao aina nyingi ambayo yanaweza kusaidia kupambana kwa kiasi kikubwa katika kuepuka utapiamlo kwa watoto.
Akizungumzia hali ya Utapiamlo katika Wilaya ya Makete kwa kipindi cha robo mwaka Afisa Lishe Wilaya Bi. Jakline Nannauka amesema hali ya Lishe ni nzuri kwa watoto waliowengi na elimu kwa wananchi inaendelea kutolewa kuhusu umuhimu wa lishe bora kwa watoto.
“Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya, hali ya lishe katika Wilaya ya Makete kwa kipindi cha robo mwaka ni nzuri na wananchi wengi wanaendelea kupata elimu kutoka kwa wahudumu wetu wa Afya kwa kutoa elimu kaya kwa kaya na kuhakisha wananchi wote wanafikiwa na elimu kuhusu Lishe hususani wanawake wajawazito”.
Mganga Mkuu Wilaya ya Makete Ligobert Kalisa amesema Wilaya ya Makete inaongoza kwa kuwa na Lishe bora kwa watoto Mkoa wa Njombe na kushika nafasi ya 16 Kitaifa jambo ambalo linaashiria hali ya lishe kuwa bora.
“Wilaya ya Makete imekuwa ya kwanza kimkoa na imeshika nafasi ya 16 Kitaifa katika suala la Lishe hivyo hatuna budi kuwapongeza Viongozi na wananchi, na Matarajio yetu robo ijayo tuwe katika nafasi nzuri zaidi Kitaifa”
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Kata ya Ikuwo Mtunyule Joachim amesema wao kama viongozi wasimamizi ngazi ya Kata watahakikisha hali ya lishe inaboreshwa zaidi katika Kata zao kwa kuongeza uwajibikaji kwa Mzazi au mlezi mwenye mtoto chini ya miaka mitano.