Watumishi wafukuzwa kazi Makete (Video)


Baraza maalum la madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Makete mkoani Njombe lililoketi kwa ajili ya kushughulikia masuala mbalimbali ya kinidhamu ya watumishi wa halmashauri hiyo pamoja na mambo mengine limeridhia kufukuzwa kazi watumishi wanne kutokana na makosa mbalimbali waliyokutwa nayo

Akizungumza na Edmo leo Septemba 28, 2022 Mwenyekiti wa Kikao hicho Mh. Atilio Ng’ondya amesema watumishi hao wanne waliofukuzwa kazi, watatu wamefukuzwa kutokana na ubadhilifu wa fedha za halmashauri na mmoja ni kutokana na utoro kazini


Amesema walikuwepo watumishi 63 wanaotuhumiwa kwa makosa mbalimbali ambapo baada ya uchunguzi imebainika watumishi 54 hawakukutwa na hatia yoyote huku watumishi 9 wakibainika kuwa na tuhuma ambapo mbali na hao wanne kufukuzwa kazi wengine kutokana na tuhuma walizonazo wamepewa onyo, wapo waliokatwa mishahara yao  asilimia 15 kwa muda wa mwaka mmoja na wengine miaka mitatu


William Makufwe ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Makete amesema iliundwa kamati ya uchunguzi ya wataalamu kutoka ofisi ya mkuu wa mkoa ambayo ndiyo ilifanya kazi yake na kutoa ripoti iliyowasilishwa kwenye baraza hilo maalum la madiwani huku asema miongoni mwa watumishi walioonekana hawana makosa  wapo waliorudisha fedha za umma walizokuwa wanadaiwa na wengine kurejesha vitabu vya serikali vya kukusanyia mapato walivyokuwa wakidaiwa


Zama za kula ama kutumia fedha za makusanyo ya serikali zikiwa chini ya usimamizi wa watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Makete zimepitwa na wakati, hivyo agizo la kukusanya fedha na kufikia shilingi laki 5 zipelekwe benki lipo pale pale ili kuepuka kujiingiza kutumia fedha za serikali pasipo utaratibu, ndio msisitizo wa Mkurugenzi Makufwe kwenda kwa watumishi wanaohusika


Watumishi waliofukuzwa kazi ni Bryson Sanga aliyekuwa Afisa mtendaji wa kijiji cha Ludihani, Godwin Luvanda aliyekuwa Afisa Mtendaji Kijiji cha Ikuwo, Tumaini Ngogo aliyekuwa Afisa Mtendaji Kijiji cha Kigala pamoja na Omega Thobias aliyekuwa Afisa Mtendaji wa Kata ya Mbalatse ambaye imeelezwa amefukuzwa kazi kwa sababu za utoro kazini kwa siku 214


Hayo yote ni matokeo ya Ukaguzi maalum uliofanywa na mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali (CAG) kwa shughuli za Halmashauri hiyo zilizofanyika kuanzia mwaka 2017/2018, 2018/2019 na 2019/2020

Video Nzima iko hapa👇👇


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo